SERIKALI imesema imebaini udanganyifu unaofanywa na wenyeji kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa kigeni Kariakoo, Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jaffo amesema kamati iliyotathmini mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wa kigeni na wazawa katika eneo hilo maarufu la biashara Tanzania, imebaini hayo.
Dk Jafo alisema hayo alipozungumza katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds cha Dar es Salaam.
Alisema kamati hiyo imesaidia kubaini mambo yaliyojificha katika sekta zingine nchini yanayofanywa na wageni.
Dk Jafo alisema imebainika kuna wazawa wanawapatia wageni taarifa zao binafsi ambazo wanazitumia katika kusajili kampuni na biashara mbalimbali kitu ambacho ni kinyume na maadili na usalama wa nchi.
“Maombi yanaonekana ni Mtanzania na eneo analoishi usajili unafanyika kampuni inafunguliwa kumbe zimetumika taarifa zake tu… jambo hili ni kosa kubwa sana na hili limeonekana kwa Watanzania wengi maduka yamefunguliwa taarifa za Mtanzania lakini mali sio za Mtanzania,’’ alisema Dk Jafo.
Alisema pia kamati imebaini kuna wageni wanaokuja kwa kigezo cha wawekezaji na wakifika nchini wanafanya shughuli zingine kinyume na usajili wao, pamoja na uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni ambao hawakuwa na sifa ya kuwepo nchini.
“Timu iliyokuwa ikifanya kazi ile imebaini kwa mfano wale wageni 31 ambao walikuwa hawana hadhi kabisa na kupitia mifumo ya kiserikali Idara ya Uhamiaji karibuni 24 walikuwa washatolewa nchini,” alieleza.
Vilevile, alisema kamati imebaini uwepo wa harufu ya rushwa kwa baadhi ya watendaji ambao sio waadilifu wanaosababisha wageni kufanya biashara kinyume na usajili wao na kutaka mifumo kuimarishwa zaidi ili kukomesha hali hiyo.
“Wakati kamati inafanya kazi ilikuwa inapokea simu kwamba usifanye hilo, usiendelee na hicho maana yake hiyo inakupa mashaka na kamati ilifanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu,” alisema Dk Jafo.
Alisema kutokana na udhaifu ambao umeonekana katika soko hilo kamati imependekeza kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Uwekezaji Namba 10 ya Mwaka 2022 pamoja na sheria inayohusu ajira za wageni Sura ya 436.
“Walivyozisoma zinatoa mianya kwa baadhi ya watu kufanya kazi nje ya utaratibu ikatoa mapendekezo kufanya marejeo ya sheria hizo kuziba mianya yote inayomfanya mtu akija hapa wakati mwingine akengeuke kutoka katika ule mstari uliowekwa,” alieleza.
Amezitaka taasisi zilizotajwa kuwa na upungufu kufanyia kazi na kuahidi kuwachukulia hatua wote ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine katika kusababisha wageni kufanya kazi kinyume na utaratibu wanachukuliwa hatua.
“Katika utekelezaji wa ripoti hii mambo makubwa yatafanyika niwahakikishie Watanzania kila mmoja atawajibika kwa kipande chake lazima muda tulikomeshe,’’ alisema.
Aidha, Dk Jaffo alisema katika kulinda bidhaa zinazozalishwa nchini, serikali imejipanga kuwezesha ujenzi
wa viwanda 9,048 ambako katika viwanda hivyo viwanda 4,156 vitakuwa viwanda vidogovidogo.
“Tunaamini uwekezaji huo utasaidia sana kuchagiza viwanda vidogo kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo baadaye tutaweka mifumo ya kikodi na sio ya kikodi lengo ni kuzuia uingizaji wa baadhi ya bidhaa ambazo tunazalisha ndani,” alisema.