Udhibiti kelele, mitetemo uwe endelevu, usiishie kwenye baa

UAMUZI wa Halmashauri Wilaya ya Kinondoni wa kufunga baa na klabu za usiku tano kwa kosa la kupiga muziki kupita kipimo kilichowekwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ni hatua muhimu inayostahili pongezi.

Hii ni ishara ya serikali na mamlaka za mitaa kujitahidi kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele hasa muziki wa usiku, ambazo zinaathiri afya ya umma, usalama na maadili ya kijamii.

Hatua hii inapaswa kuigwa na halmashauri nyingine nchini ili kuhakikisha ustawi wa wananchi na mazingira na wakati huohuo, ikiwa ni utekelezaji wa sheria.

Sheria zinazohusika na udhibiti wa kelele nchini Tanzania ni pamoja na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, ambayo inatoa mamlaka kwa Nemc na mamlaka za mitaa kudhibiti na kuzuia kelele kutokana na shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baa na klabu za usiku.

Sheria hii inakataza kelele zinazozidi kiwango kinachoruhusiwa ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na ustawi wa jamii.

Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 106 (5) imeweka bayana kwamba si ruhusa kwa mtu yeyote kupiga kelele au kusababisha kelele kuzidi kiwango kilichoainishwa au kitakachobainishwa kuhusiana na upigaji kelele.

Aidha, Kanuni za Usalama wa Mazingira zinatoa miongozo ya kupima na kudhibiti kelele, na mamlaka za mitaa zinatekeleza majukumu haya kwa kuandaa sheria ndogo za kudhibiti kiwango cha kelele katika maeneo yao.

Pamoja na sheria na kanuni kuwapo, uchafuzi wa mazingira unasababishwa na kelele na mitetemo ni miongoni mwa kero kubwa zinazohatarisha afya na mustakabali wa maendeleo ya jamii katika maeneo mengi nchini.

Kelele zinazozidi kiwango kinachoruhusiwa zimeendelea kuwapo katika maeneo mbalimbali licha ya athari zake, ikiwano huchangia matatizo ya afya kama vile kukosesha usingizi, msongo wa mawazo na kupungua kwa uwezo wa kusikia.

Ndiyo maana tunasema uamuzi wa kufungia baa na klabu za usiku wilayani Kinondoni usiwe nguvu ya soda, bali uwe endelevu pia kwa maeneo mengine nchini.

Serikali za mitaa zinalo jukumu la kuhakikisha watu wote wanaosababisha kelele wanachukuliwa hatua.

Vinginevyo, wananchi wameendelea kuchukulia kawaida kutokana na kutoona hatua za mara kwa mara zinazochukuliwa.

Kwa hiyo, ni wakati wa viongozi na mamlaka nyingine kuendeleza utaratibu wa kudhibiti kelele kwa vitendo na kuhakikisha sheria zinazohusika zinazingatiwa kikamilifu.

Udhibiti dhidi ya wachafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele zisiishie kwenye baa na klabu za usiku, bali uwe endelevu pia kwenye makazi ya watu, masoko, stendi za mabasi, nyumba za ibada na kwenye shughuli za wamachinga ambako kelele za vipaza sauti ni kero kubwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button