Ufaulu kidato cha sita juu, 71 wafutiwa matokeo

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita na mitihani ya ualimu iliyofanyika Mei mwaka huu.
Limesema waliofaulu kidato cha sita ni 125, 779 sawa na asilimia 99.95 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani.
Pia, limetangaza kuwafutia matokeo watahiniwa 71 wakiwemo ya wanafunzi wa kidato cha sita 70 na matokeo ya mwanafunzi mmoja wa mtihani wa ualimu kwa udanganyifu.
Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamedi aliwaeleza waandishi wa habari Unguja jana kuwa ufaulu umeongezeka kwa watahiniwa wa shule kwa asilimia 0.03 huku kwa watahiniwa wa kujitegemea ufaulu wao umeshuka kwa asilimia 2.64.
“Ufaulu wa jumla umepanda kwa asilimia 99.95 kwa kidato cha sita, wanafunzi 125,779 kati ya 125,847 wamefaulu kulinganisha na 2024 watahiniwa 103,252 walifaulu sawa ana asilimia 99.92,” alisema.
Aliongeza: “Kwa watahiniwa wa kujitegemea, watahiniwa 6,127 sawa na asilimia 90.7 wamefaulu huku 2024 watahiniwa waliofaulu walikuwa 7,804 sawa na asilimia 93.34 hivyo ufaulu umeshuka kwa asilimia 2.64.”
Kuhusu ubora wa ufaulu, Profesa Mohamed alisema umeongezeka kwa asilimia 0.22 huku takwimu zikionesha watahiniwa 125,375 sawa na asilimia 99.62 wamepata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu.
Alisema kati ya hao, waliopata daraja la kwanza ni watahiniwa 61,120 sawa na asilimia 48.57 na waliopata daraja la pili ni watahiniwa 49,385 sawa na asilimia 39.24 pia alisema mwaka 2024 watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 102,719 sawa na asilimia 99.40.
Kadhalika katika ufaulu kwa jinsi, alibainisha kuwa hakuna tofauti kwani wote wamefaulu kwa asilimia 99.95.
Kuhusu ufaulu katika tahasusi, waliopata daraja la kwanza na la pili katika masomo ya sayansi asilia ni asilimia 78.59 ya watahiniwa 37,067 kukiwa na ongezeko la wanafunzi 5,681 ikilinganishwa na 2024
Katika tahasusi za lugha, sayansi jamii, biashara na uchumi watahiniwa waliopata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili ni kati ya asilimia 92.25 hadi 96.35 huku asilimia 67.91 ya watahiniwa katika tahasusi za ualimu wa masomo ya sayansi na biashara wamepata daraja la tatu.
Pia, Necta ilieleza kuwa ufaulu wa shule katika umahiri unaonesha katika shule zote 977, shule 725 zimepata wastani wa daraja C, ikilinganishwa na madaraja mengine ya ufaulu.
Pia, idadi ya shule zilizopata wastani wa daraja A hadi D zimeongezeka kutoka shule 921, mwaka 2024 hadi shule 976, mwaka 2025 na shule zilizopata daraja E zimepungua kutoka shule nane mwaka 2024 hadi shule moja mwaka huu.
Kwa matokeo ya ualimu kwa ngazi ya cheti na diploma, waliofanya mtihani wa daraja A watahiniwa 6,959 sawa naa silimia 99.49 walifaulu. Walifanya mtihani wa daraja A kozi maalumu watahiniwa 681 sawa na asilimia 99.85 ya watahiniwa 682 wamefaulu.
Pia, Necta ilizuia matokeo ya watahiniwa 244 waliopata matatizo ya kiafya kwa kutofanya mitihani ya baadhi ya masomo au masomo yote hivyo watafanya mitihani yao mwakani.
Aidha, ilieleza sababu kufuta kwa matokeo ya wanafunzi 71 kuwa ni udanganyifu uliofanyika wakati wa mtihani baada ya kubaini baadhi ya wanafunzi kuwa na mfanano wa majibu, miandiko, kusaidiana, kuingia na karatasi zenye maandishi, kuingia na simu na saa janja.



