RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa Jeshi la Polisi ili kuepuka ajali za barabarani.
Ametoa maagizo hayo wakati wa kutoa pole kutokana na ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu saba na majeruhi tisa.
Ajali hiyo ilihusisha magari matatu Kijiji cha Kihanga wilayani Karagwe mkoani Kagera iliyotokea wiki hii baada ya lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 621 EJQ likiwa na tela lenye namba za usajili T 472 EAQ kugonga magari ya abiria.
Katika salamu zake juzi, Rais Samia amelielekeza Jeshi la Polisi lihakikishe madereva wanaongeza umakini, wazingatie sheria za barabarani hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Ameagiza utekelezaji wa agizo hili uende sambamba na uhuishaji na uwekaji wa alama za barabarani kwenye maeneo hatarishi, wazingatie umbali na maeneo sahihi ya uwekaji wa vituo vya ukaguzi ili vionekane kwa urahisi zaidi.
Aidha, amewakumbusha watumiaji wote wa barabara watumie namba za simu za makamanda wa polisi wa mikoa watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi wakati wowote wanapoona viashiria vya uzembe na ukiukwaji wa sheria na alama za barabarani.
Maagizo ya Rais Samia kwa mamlaka za usimamizi wa usalama barabarani ni muafaka ikizingatia kuwepo kwa ajali
za mara kwa mara zinazoendelea kutafuna roho za watu na kuwaacha wengi na ulemavu wa kudumu.
Katika ajali nyingi; iwe ni za mabasi ya abiria au magari binafsi, malori yamekuwa yakihusika kwa namna moja au
nyingine. Ama yenyewe kwa kugongwa yakiwa yamesimama barabarani au kugonga na kugongana na magari mengine.
Inawezekana zipo sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia ajali hizo, ikiwemo uendeshaji mbovu kwa maana ya kasi na kutofuata alama za barabarani, hali mbaya ya miundombinu ya barabara kutokana na kujaa maji.
Sababu nyingine inawezekana ni uchakavu wa malori, ukosefu wa mafunzo ya kutosha kwa madereva kuhusu
usalama barabarani na utunzaji wa magari pamoja na kuchoka kwa madereva hasa wa safari ndefu bila mapumziko.
Vilevile kutokana na mizigo mizito kupita kiasi inayoweza kusababisha dereva kushindwa kudhibiti gari. Hata hivyo, kwa kuwa ipo nadharia inayosema ‘bila utafiti huna haki ya kuzungumza’, tunaona upo umuhimu wa kuchunguza zaidi kubaini chanzo kikubwa cha ajali hizi na kuja na mkakati madhubuti kuzikabili.
Kwa hiyo, sambamba na mamlaka za usimamizi wa usafiri barabarani kuwajibika kuzingatia maagizo ya Rais Samia, panahitajika ukusanyaji wa data za kina kuhusu ajali mbalimbali ili kuja na majibu na mkakati endelevu ulio madhubuti.
Kwa kufanya hivyo, mamlaka zinaweza kutambua uhalisia wa ajali, zikachambua ni vipi malori au aina nyingine za magari (yaliyokithiri kwa ajali) zinavyochangia tatizo na hatua stahiki za kuchukua.
Mamlaka za usimamizi wa usafiri barabarani ziongeze juhudi katika kuweka mikakati thabiti itakayoimarisha usalama wa barabara na kuondoa hofu ya kutumia vyombo vya usafiri wa barabarani.