WATU watano wamefariki Dunia na wengine wawili wakiwa hospitalini baada ya kuibuka kwa ugonjwa ambao bado haujajulikana huko Bukoba vijijini mkoani Kagera, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof.
Tumaini Nagu amesema.
Serikali imetoa tahadhari kwa umma kuwa ugonjwa huo umejitokeza katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega, kata ya Maruku na Kanyangercko wilaya ya Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.
Prof. Nagu amesema mjini Dodoma kuwa jumla ya watu 7 wanasadikika walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.
Amesema kuwa watu watano kati yao wamefariki na wengine wawili wako hospitali wanaendelea na matibabu.
“Mwenendo wa ugonjwa huu unaashiria uwezekano kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza hivyo Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na kuchukua hatua za kudhibiti ili usisambae,” amesema Prof.
Nagu.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Nagu akizungumza na Waandishi wa Habari Dodoma juu ya tahadhari ya ugonjwa usiojulikana KageraAidha, Prof. Nagu amewataka wananchi kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu endapo ataona dalili kama kupatwa na homa, kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu.
Pia, amewakumbusha kuwahi Kutoa taarifa mapema kwenye kituo cha kutolea huduma kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bila malipo endapo utamuona au kukutana na mtu mwenye dalili kama hizo.
“Mnatakiwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza,” amesema Prof. Nagu
Pia, amewataka wananchi Kushirikisha wataalamu wa afya katika shughuli za misiba na mazishi katika kipindi hiki, kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.
Mwisho, amewakumbusha watumishi wa afa kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza (IPC) wakati wa kutoa huduma.