Ugumu mikopo wanaotoka shule binafsi wahojiwa
Mbunge wa Viti Maalum Sophia Mwakagenda amehoji kuhusu ugumu wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi wanapojiunga na elimu ya juu.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Juma Kipanga, amesema mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini, hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu.
“Aidha, upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) kwa kuzingatia sifa za msingi ambazo ni: Awe Mtanzania; Awe amepata udahili wa masomo ya shahada au stashahada katika taasisi inayotambuliwa na Serikali; Asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake; na kwa wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, watatu na kuendelea, wawe wamefaulu kuendelea na masomo yao katika mwaka unaofuata.
“Mheshimwa Spika, Kila mwaka Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika.
“Pamoja na vigezo vilivyotajwa, mwongozo huelekeza taratibu za kufuata wakati wa kuomba mkopo pasipo kuangalia mwanafunzi kasoma shule ya binafsi au ya umma.
“ Mheshimiwa Spika, iwapo muomboji atafuata maelekezo yote kama yalivyo katika mwongozo wa mwaka husika na akawa ana vigezo vyote, hatutegemei pawepo na ugumu wowote katika kupata mkopo hata kama alisoma shule binafsi,” amesema Naibu Waziri.
–