Ujenzi wa miundombinu wazalisha ajira uchukuzi

DODOMA: Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema katika kukuza upatikanaji wa ajira nchini, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kutoa ajira 198,480 wakati wa ujenzi wa miundombinu pamoja na utoaji wa huduma za uchukuzi.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo Mei 13, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema sekta hiyo imeendelea pia kuchangia katika upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma za uchukuzi, usafirishaji na huduma za bandari.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2025, sekta ya uchukuzi ilichangia mauzo ya huduma yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.79, ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.35 zilizochangiwa mwaka 2024.
Prof. Mbarawa amesema mafanikio hayo yanaonesha namna sekta ya uchukuzi inavyoendelea kuwa mhimili muhimu katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira na kuimarisha mapato ya fedha za kigeni nchini.



