Ujenzi wa shule Chinyonyo wapamba moto
WANANCHI wa Mtaa wa Chinyoyo, Kata ya Kilimani Jijini Dodoma wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini.Anthony Mavunde kwa ujenzi wa shule mpya ya msingi Chinyoyo.
Kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kuwapunguzia watoto kero ya kutembea umbali mrefu kufuata shule Kata za jirani.
Akitoa maelezo ya awali Diwani wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko amesema wanafunzi wengi wanaotoka eneo hilo la Chinyoyo wanatembea umbali mrefu kufuata shule katika kata za jirani ambapo imekuwa ni kero kubwa kwa watoto hasa wa kike ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali wakiwa njiani.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ambaye ndio alizindua zoezi la uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa madarasa hayo amesema eneo hilo limekuwa na changamoto ya kuwa na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo shule.
“Kutokana na historia ya eneo hili palitengwa kuwa ukanda wa kijani kwa ramani ya 1976 kabla hapajabadilishwa matumizi na kuwa sehemu ya makazi miaka ya hivi karibuni baada ya kumalizika kwa mgogoro wa ardhi wa muda mrefu.
“Nilikuja hapa miezi kadhaa iliyopita wa mwaka huu nikawaahidi wananchi kwamba tutaanza ujenzi wa shule ndani ya mwezi Julai,2023, leo nimefurahi ahadi imetimia na tumeanza kuchimba msingi kwa kushirikiana na wananchi.” Amesema
Amesema, ujenzi huo utahusisha madarasa manne ya hatua ya awali ambapo jumla ya sh milioni 80 zimetolewa na serikali chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Pia, ofisi ya Mbunge pia itajenga darasa moja katika kuunga mkono jitihada hizo zitakazosimamiwa you have za serikali na wananchi ili kuboresha elimu katika mtaa wa Chinyoyo.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa CCM Kata ya Kilimani, Katibu wa CCM Kata, Lotary Ndimbo amepongeza jitihada za serikali na viongozi katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM 2020/2025 na kutaka ujenzi huo usimamiwe vizuri ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi.