Ukarabati Songo Songo kupaisha uzalishaji gesi asilia

Ukarabati Songo Songo kupaisha uzalishaji gesi asilia Ukarabati Songo Songo kupaisha uzalishaji gesi asilia

LINDI: Ukarabati wa kisima cha gesi asilia unaoendelea katika Kitalu cha Songo Songo mkoani Lindi unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 20 kwa siku.

Ujazo huo unaweza kusaidia uzalishaji takribani megawati 100 za umeme.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika kitalu hicho mnamo Oktoba 26, 2024.

Advertisement

Mhandisi Sangweni alieleza kuwa kisima kinachofanyiwa ukarabati (SS7) kilipata changamoto ya kiufundi, hali iliyopelekea uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika kisima hicho kusitishwa kwa muda.

Kwa mujibu wa maelezo ya Sangweni, ukarabati huo utagharimu takribani Dola za Marekani Milioni 20 na unatarajiwa kukamilika mapema mwezi ujao.

SOMA: Wizara yaitaka PURA kujipanga utangazaji vitalu vya mafuta, gesi

“Ongezeko la futi za ujazo milioni 20 kwa siku unaotarajiwa mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wa kisima hiki unaweza kuzalisha mpaka megawati 100 za umeme,” aliongeza Sangweni.

Uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika Kitalu cha Songo Songo ulianza mwaka 2004 kwa lengo kuu la kuzalisha umeme.

Kwa sasa, Kitalu hicho kina jumla ya visima sita vinavyozalisha gesi asilia. Visima hivyo ni SS3, SS5, SS9, SS10, SS11 na SS12.

Kwa robo ya kwanza ya mwaka 2024/25, uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika Kitalu cha Songo Songo ulikuwa wa wastani wa futi za ujazo milioni 86 kwa siku.