Ulega aiagiza TBA ujenzi nyumba za gharama nafuu

 DAR ES SALAAM: Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kufanya tathmini ya uwezekano wa kujenga nyumba za kupangisha kwa ajili ya wananchi wa kipato cha kati na cha chini.

Maagizo hayo yanalenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora na yenye gharama nafuu, hasa katika maeneo ya mijini ambako mahitaji ya nyumba yanaongezeka kwa kasi.

Aidha, hatua hiyo pia inatarajiwa kusaidia kuimarisha sekta ya ujenzi na kuchochea ajira na ukuaji uchumi kupitia uwekezaji wa miradi ya makazi.

Ulega alitoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wenye wajumbe watano akiwemo Mwenyekiti, Dk Laurean Ndumbaro na katibu wake Dar es Salaam jana.

“Ongezeni kasi, tafuteni maarifa, shirikianeni na mabenki, jengeni majengo ya pesa nyingi, ya wateja wenye pesa nyingi, ila jengeni majengo ya gharama nafuu ya watu wa tabaka la chini,” alisema Ulega.

Alisema dhamira ya serikali ni kuona sekta ya ujenzi inakuwa chanzo cha ukuaji wa ajira, uchumi na ustawi wa wananchi wake.

Ulega alisema taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, ikiwemo TBA, zinapaswa kufanya kazi kwa ubunifu na uwajibikaji ili kutafsiri malengo ya Dira ya Kisera kuwa matokeo chanya.

Alisema serikai inakusudia kufikia ujenzi wa makazi bora 50,000 ifikapo mwaka 2030. Hivyo TBA wana jukumu la kusimamia ujenzi wa nyumba 4,500 kuendelea na kukarabati majengo ya serikali yaliyopo, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi ya mali za serikali.

Aidha, kabla ya uzinduzi wa bodi hiyo, Waziri Ulega alikagua ujenzi wa nyumba tatu mpya za ghorofa zilizojengwa na TBA Masaki Dar es Salaam. Nyumba hizo zimejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 13 fedha za ndani kutoka kwa wakala huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button