Ulega ataka kasi ujenzi miundombinu Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, Dodoma ukamilike haraka.

Ulega ametoa agizo hilo Dodoma baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya urefu wa kilometa 112 ambayo kwa sasa imefikia asilimia 85.

Pia, alikagua barabara za kutua na kurukia ndege na jengo la abiria kwenye kiwanja hicho.

Ulega alisema serikali inaendelea na mpango wa kuhakikisha inapunguza msongamano Dar es Salaam na Jiji la Dodoma kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara za juu za Mwenge na Morocco, Dar es Salaam na ujenzi wa barabara sita kwa nne kuanzia katikati ya Dodoma kwa njia ya kwenda Dar es Salaam -Iringa -Arusha.

Ulega amemuagiza mkandarasi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato aongeze wafanyakazi na afanye kazi mchana na usiku ili ujenzi huo ukamilike kwa muda uliopangwa katika mkataba ambao ni Novemba 30, mwaka huu.

“Nimeagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na TANROAD (Wakala wa Barabara Tanzania) kufanya kazi kwa pamoja katika kumsimamia mkandarasi huyu kwa sababu tusiache upande mmoja. Tunachotaka kuona kama Watanzania mradi huu ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa,” aliagiza Ulega.

Ulega alisema ofisi yake haitaongeza muda katika ujenzi huo ikiwa mkandarasi huyo atafanya uzembe watamdai fidia ya kuchelewesha mradi.

“Na natoa maelekezo kwa miradi yote wanapochelewa hasa katika ile miradi ambayo tuna uhakika kuwa tunazo fedha lazima tuwadai fidia wanapochelewa ni kama wale wa Dar es Salaam wa BRT (Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Kasi) wote nimewaambia wawadai fidia hatuna kesi ya masuala ya fedha pale,” alisema.

Ulega aliwataka wataalamu wa Tanroads wafanye usimamizi wa karibu kwa wakandarasi ili barabara ya mzunguko Dodoma ikamilike kwa wakati.

“Wakandarasi ongezeni kasi ya ujenzi huku mkiongeza idadi ya wafanyakazi, vifaa na muda wa kufanyakazi kwa
kufanyakazi za ujenzi usiku na mchana,” alisema.

Ulega alisema barabara hiyo itasaidia kuuandaa mji wa Dodoma kuwa na barabara za kisasa na usiwe na msongamano wa magari.

Aliagiza Tanroads wahakikishe njia za watembea kwa miguu zinakamilika, bustani za miti zinapandwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button