Ulega: Samia ameinua Wizara ya Mifugo na Uvuvi
DAR ES SALAAM: Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameisaidia wizara hiyo kwenye upande wa Bajeti mara nne zaidi yabajeti waliyokua nayo kwa mwaka 2021/2022.
Ulega amesema hayo leo Machi 27 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam katika kilele cha kurasa 365 za Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema mwaka 2021/2022 Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilikua na bajeti ya Sh bilioni 66.5 ambapo kwa sasa bajeti yao ni Sh bilioni 295.9 ikiwa ni mara nne zaidi.
Amesema ongezeko la bajeti hiyo imeisaidia wizara hiyo kupiga hatua kwenye utendaji wa kazi ambapo kwa sasa Tanzania imefanikiwa kupeleka nyama nchi kama za Dubai na Saudia kitu ambacho miaka ya nyuma hakikuwahi kuwepo.
Ulega, amesema pia ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Lindi umefikia asilimia 52 ambao ujenzi wake utatumia gharama ya Sh bilioni 289 ikiwa na lengo la kufungua uchumi wa Buluu.
Amesema, mradi wa Building Better Tomorrow (BBT) kwa upande wa Mifugo na Uvuvi imefanya kazi nzuri kwenye vituo nane na sasa vinaenda kuwa vituo 13 ambapo walinunuliwa ng’ombe 2,348 na waligawanywa kwenye vituo nane ikiwemo Tanga, Mwanza na Kagera na tayari faida ya zaidi ya Sh milioni 100 imepatikana kwenye mradi huo wa BBT.
Aidha, amesema minada 51 imejengwa yenye thamani ya Sh bilioni 17.5 na ng’ombe zaidi Sh milioni 12 imeuzwa kwenye minada hiyo, na tayari wizara imepata ithibati ya mbegu za malisho ambazo wafugaji wataenda kununua kwa ajili ya kipindi cha kiangazi ili wafugaji wasikose malisho.