WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa siku saba kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kupeleka vifaa tiba na mashine ya usingizi na upasuaji katika kituo cha afya cha Kabyaire kilichopo wilayani Misenyi.
Ummy ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo na mwenendo wa udhibiti wa ugonjwa wa Ebola katika kituo hicho, ambacho kipo kilomita 70 kufika Mubende nchini Uganda.
Mubende ndio Wilaya iliyokumbwa na mlipuko mkubwa wa Ebola, ambapo mpaka sasa Uganda imeripoti vifo 30 na wagonjwa 43.
Kituo hicho cha Kabyaire, ndicho kilichotengwa maalumu kwa matibabu kwa wagonjwa wa Ebola.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Ummy amesema watatekeleza maagizo yote yanayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa upande wa huduma za afya inajikita kwenye ubora wa huduma, hivyo vifaa tiba tutaleta maana yake atakapotokea mgonjwa wa Ebola na anatakiwa kufanyiwa upasuaji iwe rahisi kumuhudumia,” alisema.
Amewataka watumishi wa afya hususani viongozi kusema ukweli kwamba dawa hazipo na hivyo kuwataka kuboresha huduma katika vituo vyao, ili kutatua changamoto zilizopo na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, ikiwemo dawa na vifaa tiba.
“Mseme ukweli kama vifaa tiba hamna mseme, kama dawa hamna mseme msifanye siasa, semeni kweli ili changamoto zilizopo zitatuliwe, siasa tuachieni sisi wanasiasa,” amesema.