Umoja wa Mataifa waunga mkono kilimo cha umwagiliaji

MRATIBU Mkaazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Zlatan Milisic amesema umoja huo unaunga mkono ajenda ya serikali ya kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji hivyo, watahakikisha rasilimali za maji zinapatikana kwa wale wanaohitaji kupitia programu mbalimbali.

Amesema mabadiliko ya hali ya hewa, ongezeko la idadi ya watu, ukuaji wa miji, ukuaji wa viwanda, na maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii yanaongeza mahitaji ya rasilimali za maji na chakula.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa rasilimali hiyo, Milisic amesema “Zaidi ya 1/3 ya watu duniani hawana maji salama ya kunywa, wakulima wadogo wadogo, hasa wanawake na vijana ni waathirika wakubwa kwani wamekuwa wakihangaika kukidhi mahitaji yao ya kila siku.”

Pia ameeleza kuwa uhaba wa maji ni changamoto ya kimataifa ambayo inahitaji kila nchi kuchukua hatua na kwamba wana jukumu la kupunguza upotevu wa maji na kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na ujenzi wa mifumo ya umwagiliaji ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Milisic amesema kuwa ni vema kuhakikisha usalama wa maji katika kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu hivyo, utafiti na matumizi ya teknolojia utatoa suluhu mpya na endelevu katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa maji, usimamizi na mifumo ikolojia iliyoharibiwa.

Mratibu huyo amesisisitiza kuwa ni muhimu kuwapatia wakulima zana, ujuzi, na teknolojia sahihi kwa ajili ya mbinu endelevu za kilimo ambazo ni rafiki kwa mazingira, kutumia maji kwa ufanisi zaidi na kutoa ulinzi bora dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.

“Hatua zaidi zinahitajika ili kupunguza uharibifu unaotokana na matumizi ya viuatilifu hatari kwa kuboresha ubora wa maji na kupunguza hatari za usalama wa chakula kuanzia shambani, ili kuzuia uchafuzi wa chakula,” alisema.

Aidha, ameeleza kuwa “Tunaipongeza serikali kwa kuongeza bajeti katika kilimo cha umwagiliaji kwani itaongeza usalama wa chakula na kustahimili majanga mbalimbali yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.”

Amesema bajeti kwa ajili ya skimu za umwagiliaji iliongezwa kutoka Dola za Marekani milioni 181 katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 20 pekee mwaka uliopita kwamba italeta manufaa makubwa, hasa katika kuhakikisha kuwa wakulima wadogo wanapata maji.

“Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali, wakulima, jamii na wadau wengine kubadilisha mifumo ya kilimo cha chakula ili kuongeza uzalishaji utakaochochea lishe bora, mazingira bora na maisha bora kwa wote Ili kutomwacha mtu nyuma,” amesisitiza Milisic.

Pia amesema kuwa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, na wadau wote wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba mifumo ya chakula inazalisha aina mbalimbali za vyakula kulingana na idadi ya watu inayoongezeka.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x