Umuhimu wa Baraza Huru la Habari na changamoto zake

TASNIA ya sheria nchini inaadhimisha Wiki ya Sheria iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango Januari 22, 2023, Dodoma na itahitimishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Kaulimbiu ya Siku ya Sheria mwaka huu imejikita zaidi katika msisitizo wa Mahakama kutumia usuluhishi kama njia rahisi ya kutatua migogoro ya jamii na hata kampuni au taasisi zinazotafuta haki mahakamani.

Jaji Mkuu, Makamu wa Rais na watendaji wengi wa Mahakama wametoa rai kwa wadau wa sheria kutumia usuluhishi kama njia ya haraka ya kutatua migogoro kati yao, isiyogharimu fedha nyingi, inayoacha jamii na amani badala ya chuki kati yao.

Kaulimbiu hiyo imekuja wakati mwafaka ambapo mmoja wa wadau wa sheria nchini, waandishi wa habari wakipigania haki ya tasnia yao kutambuliwa kwa sheria ya Bunge itakayowapa fursa ya kuwa na Baraza Huru la Habari litakalosimamia taaluma yao.

Tayari Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na taasisi za habari wamewasilisha serikalini, randama inayopendekeza mabadiliko ya sheria za habari ambazo zimekuwa si rafiki kwa wanahabari nchini.

TEF wanataka Baraza Huru la Habari badala ya tasnia yao kuendelea kusimamiwa na taasisi tatu tofauti chini ya sheria ya sasa ya MSA, 2016. TEF inapendekeza Baraza la Ithibati, Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari na Baraza la Habari Tanzania ziunganishwe iwe Baraza Huru la Habari Tanzania

TEF inadai sheria za sasa za habari zinaipa serikali dhamana kubwa mno ya kusimamia uendeshaji wa vyombo vya habari kupitia taasisi zake kama Idara ya Habari Maelezo ambapo Msajili anaweza kufuta, kufungia au kuzuia gazeti kuchapwa atakavyo yeye.

Je, hoja ya TEF ina mashiko? Jibu ni ndio kwani uzoefu unaonesha nchi nyingi duniani zimeanza kuiacha tasnia ya habari ijisimamie ingawa ujio wa teknolojia za kidijiti, mitandao ya kijamii, luninga n.k inaacha mjadala kuhusu udhibiti usio na mipaka.

TEF inasema tasnia yao kama walivyo wanasheria (TLS), wakandarasi (CRB), wahasibu (NBAA), walimu (CWT), mabaharia ikisimamiwa na chombo kimoja, ufanisi utakuwa mkubwa, itapunguza gharama za uendeshaji, itadhibiti mgongano wa kitaasisi wa usimamizi na itastawisha mawasiliano ya taasisi.

TEF inatoa mfano wa nchi ambazo wanahabari wanasimamia tasnia yao ni Kenya kupitia Baraza lao la Habari, Canada (Tume ya Radio-Televisheni na Mawasiliano), Ghana (Tume ya Habari ya Taifa).

Hoja ya TEF tasnia ya habari kujisimamia inaungwa mkono na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma aliyewaambia waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuwa na baraza lao la kitaaluma litakalosuluhisha kesi zote zinazohusiana na malalamiko kuhusu taaluma yao.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Wiki ya Sheria 2023 Dar es Salaam hivi karibuni, Jaji Mkuu alisema Baraza la sasa la Habari (MCT) limefanya kazi nzuri ya kusuluhisha migogoro ya wanahabari hivyo kuna umuhimu wa kuwa washirika wakubwa wa Siku ya Sheria nchini.

Jaji Mkuu anasema, waandishi kupelekana barazani hupunguza gharama za madai, muda kushughulikia matatizo na kufanya mdai na mdaiwa waendeleze uhusiano baada ya shauri kinyume na mahakamani.

Mwandishi mkongwe, Wakili Aloyce Komba anaunga mkono wanahabari kuwa na chombo huru kilichopo kwa mujibu wa Sheria ya Bunge badala ya kutambulika mhimili wa nne wa dola kinadharia tu.

“Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18 na 19 zinatambua uhuru wa kujieleza, kutoa mawazo lakini hakuna sheria ya Bunge inayowapa nguvu waandishi kutambulika kisheria kama wanasheria, madaktari hivyo kukosa ulinzi kikatiba,” anasema.

Anasema waandishi wakitambulika kwa sheria ya Bunge, watasimamia masuala yao ya weledi na utendaji kazi na wanapokosea, kuadhibiana kupitia kamati za maadili kama ilivyo kwa mawakili TLS.

Kuthibitisha uzuri wa wanataaluma kujidhibiti, Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Zainab Chaula aliwahi kuwaambia wahariri Msajili wa Chama cha Madaktari ni daktari ingawa kajiongeza kusoma sheria aweze kutatua kesi kwa weledi zaidi.

Athari ya kesi za waandishi kupelekwa Mahakama Kuu inajionesha katika shauri la Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe dhidi ya mwanahabari, Cyprian Musiba ambaye ametakiwa kulipa fedha nyingi.

Mwandishi wa zamani wa Daily News na Wakili mstaafu wa Benki ya CRDB, Solanus Ndunguru naye ameunga mkono wanahabari kuwa na baraza lao kama chombo cha kusimamia taaluma yao lakini akaonya baraza hilo liendeshwe kwa mfumo mzuri.

Kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kuwa huru, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Gutterrez amekuwa akitetea uhuru wa vyombo vya habari akisema kazi yao ni muhimu kwa jamii kama ilivyothibitika wakati wa Covid-19.

“Duniani kote, uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu na haki za binadamu. Ni nguzo muhimu kwa ajili ya ujenzi wa taasisi zenye haki na zisizo na upendeleo,” alisema Gutterrez akipongeza waandishi walioshinda tuzo za Nobel, Maria Ressa na Demirty Muratov.

Unesco pia inaeleza umuhimu wa chombo huru cha wanahabari kama lisemavyo andiko lake la Umuhimu wa vyombo vya habari kujisimamia ili kulinda uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka 2019.

Andiko linaeleza faida za waandishi kujisimamia kuwa ni kutatua kesi au mashauri kwa usuluhishi kabla ya wadaawa kufikishana mahakamani ambako mshindi hupewa ushindi na kujenga chuki kati yao.

Pamoja na TEF kutaka baraza huru, hoja yake ina changamoto kubwa katika nchi nyingi kutokana na serikali za nchi nyingi kutaka kuendelea kudhibiti sekta hiyo kwa manufaa yake kisiasa, kiuchumi, ulinzi katika masuala yanayogusa usalama wa nchi.

Ni kwa sababu hiyo, baadhi ya serikali duniani haziamini katika uwepo wa uhuru kamili wa vyombo vya habari. Mkurugenzi wa zamani wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu aliwahi kuwaambia wahariri Dar es Salaam 2022, hakuna kitu kama ‘uhuru kamili’ wa habari duniani.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC One), Dk Ayoub Ryoba alisema katika mkutano wa wadau wa habari Dar es Salaam Desemba 2022, uhuru wa wanahabari kujisimamia hautakuwa na maana kama hawatatumia uhuru huo kutenda kwa kutoa habari zenye maslahi kwa nchi kama kufichua maovu kusaidia viongozi wa serikali.

Ni wazi kwa kurejea angalizo la wadau hao, safari ya waandishi ‘kujisimamia kwa asilimia 100 ni ndefu kwani uzoefu unaonesha udhibiti wa maudhui ya mitandao ya kijamii na baadhi ya matangazo ya kibiashara katika TV na intaneti ni mgumu na bado unazua mjadala. Lakini kuundwa chombo chao kutapunguza malalamiko ya waandishi kudhibitiwa na dola.

Mfano wa wanahabari kushughulikiwa na chombo chao ni ‘ombudsman’ ya waandishi wa Marekani inayosuluhisha malalamiko dhidi ya wahariri au ya Bosnia na Herzgovina ambako hakuna kushitaki mahakamani bali katika baraza ambako waandishi huadhibiwa kwa kuomba radhi mtu waliyemkosea.

Botswana, Zambia zimepigania pia kuwa na mabaraza yanayojisimamia, Zimbabwe ikihangaika kuungana na nchi hizo katika kutaka vyombo vyake vya habari kujisimamia. Hata hivyo, hatua kama hizo zimekuwa zikikutana na changamoto za wanasiasa kutaka kulemaza jitihada zinapochipuka.

Mfano Mhariri wa gazeti la Daily Mail la Uingereza aliyewahi kuwa Mkuu wa Taasisi ya wanahabari ya Ofcom, aliwahi kutangazwa kuteuliwa kumsaidia Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na kuzua mjadala wa umakini na uhuru wa taasisi hiyo kama mmoja wa maofisa wake anakubali uteuzi wa kisiasa wa kiongozi wa nchi.

Ingawa uingiliaji wa wanasiasa inabaki kuwa moja ya changamoto, TEF ina bahati kuwa katiba yake na hata ya nchi haizuii waandishi kuteuliwa serikalini na nzuri zaidi ni kuwa, Rais Samia anaunga mkono uhuru wa vyombo vya habari.

Tayari Rais Samia ameteua waandishi kadhaa wa habari kuwa wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu wakuu kuthibitisha anavyoienzi tasnia hiyo na kumwagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, kusimamia uhuru wa vyombo vya habari kwa kupeleka muswada wa sheria mpya ya habari bungeni.

Hata hivyo, wanataaluma watakapogoma kulitumia baraza huru, Jaji Mkuu Profesa Juma anasema mahakama bado iko wazi kwa wasiotaka kufuata usuluhishi MCT au baraza huru lijalo.

Pamoja na changamoto hizo, umuhimu wa uwepo wa baraza huru ni mkubwa na itapendeza wabunge wakiupitisha muswada utakaowasilishwa na Waziri Nape ili kuwezesha kufunguliwa kwa ukurasa mpya.

Hata hivyo, kupitishwa kwa sheria mpya itakayotoa fursa ya wanahabari kujisimamia kunapaswa kwenda sanjari na wanahabari kuzingatia sheria za habari na nchi kama Rais Samia alivyowataka Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari 2022 Arusha akionya kuwa, atakayevuka mipaka na ‘kumpara’, ‘atamparura’ pia.

Mwisho

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili.

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button