UN yaipongeza Tanzania uhuru vyombo vya habari

MWAKILISHI Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini (UN), Susan Namondo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.
Namondo alitoa pongezi hizo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa pili wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Barani Afrika (NIMCA) uliofunguliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Kituo cha Mikutano cha Kitaifa Arusha (AICC) jijini Arusha jana.
Mkutano huo umefanyika sanjari na maadhimisho ya miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Namondo alipongeza juhudi zinazoendelea nchini katika kuhuisha sheria za habari na mawasiliano ili kuimarisha uwazi, kulinda uhuru wa habari na kuimarisha imani ya umma kwa uandishi wa habari.
Alisema Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi ya kisheria hivi karibuni ikiwemo mabadiliko katika sheria ya uhalifu wa mtandaoni na sheria ya huduma za vyombo vya habari.
“Tunaipongeza Tanzania kwa kujali uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo kuheshimu miiko ya taaluma zenu lakini pia kuheshimu utamaduni wetu,” alisema.
Pia, alisifu ushirikiano mzuri uliopo kati ya MCT na serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuboresha sera za vyombo vya habari.
Aidha, alisema mkutano huo umeleta pamoja wadau wa habari kutoka barani Afrika kwa lengo la kuimarisha mazingira ya vyombo vya habari, kukuza uhuru wa vyombo vya habari, kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na kuimarisha mchango muhimu wa vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii.
“Kwa uelewa wangu, jukumu la msingi la mabaraza ya habari, au vyama vya wanahabari, kama wanavyoitwa katika baadhi ya nchi, ni kudhibiti na kusimamia mienendo ya vyombo vya habari ndani ya mamlaka yao, mabaraza ya vyombo vya habari yanatarajiwa kuhakikisha uwajibikaji, kushughulikia masuala ya kimaadili na kulinda maslahi ya taaluma ya uandishi wa habari, kwa kutekeleza majukumu haya, mabaraza ya vyombo vya habari yanatekeleza majukumu muhimu ya uandishi wa habari katika kuinua kiwango cha imani ya umma,”alisema Namondo.
Aliongeza: “Mabaraza ya vyombo vya habari yana wajibu wa kupokea na kuchunguza malalamiko yanayohusiana na ukiukwaji wa maadili na kusimamia au kupendekeza hatua zinazofaa. Mabaraza ya vyombo vya habari na mashirika ya habari nyakati hizi yanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaathiri kwa kiasi kikubwa taaluma, uaminifu na ufanisi wake kwa ujumla, na muhimu zaidi kati ya hizo ni mmomonyoko wa uaminifu wa umma”.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Taifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) anayehusika na habari na mawasiliano, Dk Tawfik Jelassi alisema kuwa sekta ya habari barani Afrika inakabiliana na kuenea kwa taarifa potofu na upotoshaji, ongezeko la kutoaminiana kwa taasisi na kuendelea kuwepo kwa uwakilishi mdogo wa jamii zilizotengwa jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi haraka.



