UNDP yatoa milioni 70 kukuza biashara

WANAFUNZI wajasiriamali 20 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini wamepatiwa zaidi ya Shilingi milioni 70 kwa ajili ya kukuza biashara zao, baada ya kuibuka washindi katika shindano la uwasilishaji wa mawazo ya biashara lililoandaliwa chini ya mpango wa Youth Ignite Student Founders Fellowship awamu ya pili.

Mpango huo unatekelezwa kupitia Programu ya FUNGUO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania, kwa ufadhili wa pamoja wa Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Finland.

Shindano hilo liliwakutanisha wanafunzi 30 kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, waliowasilisha mawazo bunifu ya biashara yenye mchango chanya kwa jamii mbele ya jopo la majaji, hatua inayolenga kukuza ujasiriamali na ubunifu miongoni mwa vijana. Mbali na zawadi za fedha, washiriki walipatiwa pia msaada wa kitaalamu ikiwemo mafunzo ya maendeleo ya biashara, ushauri elekezi (mentorship) na maandalizi ya kuwawezesha kuvutia wawekezaji wapya.

Akizungumza na HabariLeo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Harun Makandi, amesema mpango huo unaendana na jitihada za serikali za kukuza ubunifu, utafiti wenye tija kibiashara na ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, John Rutere, amesema programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kupitia uwekezaji wa kimkakati kwa vijana na biashara zao. Washirika wa maendeleo wamesema uwekezaji katika biashara zinazoongozwa na vijana ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi jumuishi.

Taasisi za Westerwelle Foundation Tanzania na StartHub Africa zimetajwa kutoa mafunzo ya vitendo ya ujasiriamali na uwasilishaji wa mawazo ya biashara kabla ya mashindano hayo. Miongoni mwa washindi waliopokea Shilingi milioni sita kila mmoja ni Herriet Nairumbe, mwanzilishi wa Niches Food Products kutoka Arusha, anayejihusisha na uongezaji thamani wa mazao ya pilipili na matunda.

Mshindi mwingine, Irene George ambaye mwanzilishi mwenza wa Eco Mushroom, amesema ufadhili huo utamsaidia kuboresha miundombinu ya uzalishaji, kuongeza ajira kwa vijana na kupanua wigo wa soko, baada ya biashara yao kukumbwa na changamoto ya kushindwa kukidhi mahitaji ya oda kubwa. SOMA: Tanzania kuendeleza ushirikiano na UNDP

Mpango wa Youth Ignite Student Founders Fellowship unaendelea kujenga kizazi cha wajasiriamali vijana wenye uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara endelevu katika sekta mbalimbali zikiwemo teknolojia, kilimo-biashara, mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji viwandani na ubunifu wa kijamii, hatua inayochangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button