Uongozi mpya SRT urejeshe mafanikio ya riadha nchini

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (SRT) hivi karibuni lilifanya uchaguzi wake mkuu jijini Mwanza na kupata viongozi wake wapya watakaoongoza kwa muda wa miaka minne ijayo.
Kwa muda mrefu wadau wa mchezo wa riadha nchini wamekuwa wakilalamika kuhusu kuchelewa kufanyika kwa uchaguzi huo na kuendelea kuwaweka zaidi madarakani viongozi waliokuwepo.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kumewezesha kupatikana kwa viongozi wapya, wakiongozwa na Rais mpya wa SRT, Rogath Stephen ambaye ni mwanariadha wa zamani na kocha wa mchezo huo hapa nchini.
Kilio cha wadau ni kama kimesikika, kwani kwa muda mrefu walitaka SRT iongozwe na waliowahi kukimbia, yaani wanaridha wa zamani ambao ndio wanajua uchungu wa mchezo huo.
Sasa ndoto zimetimia kwa kiongozi mkuu wa shirikisho hilo kuwa ni mwanariadha wa zamani na alikuwa katibu mkuu wa chama cha riadha Mkoa wa Arusha, ilipo kambi ya wanariadha wengi wa Tanzania, hasa wale wanaofanya vizuri kimataifa.
Uongozi wa shirikisho la riadha umeshapatikana, sasa wadau wengi wa mchezo huo wanasubiri riadha kurudi enzi za akina Filbert Bayi, Juma Ikangaa na wengine wengi waliofanya vizuri wakati huo Tanzania ilipong’ara katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Kwanza, tunaipongeza safu yote ya uongozi wa SRT iliyochaguliwa ikiongozwa na Rais Rogath Stephane, naibu wake Jackson Ndaweka na wengine, ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Ukiondoa katibu mkuu na mhazini, wote waliobaki ni viongozi wakujitolea kwa mujibu wa Katiba ya shirikisho hilo na wanalijua hilo, hivyo kila mtu afanye majukumu yake ipasavyo kwa jinsi alivyoomba kura kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi.
Makundi yaliyokuwepo wakati wa uchaguzi yavunjwe na wote muwe kitu kimoja ili kulisukuma vyema gurudumu la maendeleo ya mchezo huo hapa nchini, baada ya muda mrefu kushindwa kutwaa medali kutoka katika Michezo ya Olimpiki.
Wadau wa mchezo wa riadha tuwape muda viongozi hao wapya ili waweze kufanya kazi kwa weledi kuleta maendeleo ya mchezo huo yaliyopotea kwa muda mrefu.
Medali za Michezo ya Olimpiki, Tanzania ilizipata mwaka 1980 kutoka kwa Bayi aliyeshika nafasi ya pili ya mbio za meta 3,000 kuruka gogo na maji na nyingine ni ile ya meta 5,000 kutoka kwa Suleman Nyambui naye alishika nafasi ya pili. Michezo hiyo ilifanyikia Moscow, Urusi.
Hadi ikifika mwaka 2028 itakapofanyika olimpiki nyingine itakuwa ni miaka 48 tangu Tanzania ilipopata kwa mara ya kwanza na mwisho medali hizo za Olimpiki.
Uongozi mpya wa SRT moja ya jukumu lenu ni kuhakikisha mnawezesha wanariadha wetu kuleta medali za Olimpiki kwa kuandaa vijana wazuri watakaoleta maajabu.
Pia tumaini la wengi ni kufufua michezo ya mbio fupi na za kati, ambazo zimepotea kabisa na sasa kila mwanaridha anataka kukimbia mbio za marathoni tu na waandaaji nao kila kukicha wanataka kuandaa mbio hizo ndefu, kama zingine hazipo.
Uongozi mpya wa SRT fanyeni kazi kwa weledi, kwani shirikisho lenu lina matatizo mengi yanayohitaji uamuzi mgumu ili kuyatatua.



