Urais wa Denmark wa Baraza la EU na manufaa Afrika
TANGU Julai hadi Desemba 2025, Denmark inashika nafasi muhimu ndani ya Umoja wa Ulaya.
Hiyo ni nafasi ambayo huenda watu wengi nje ya Ulaya hawaifahamu, lakini ni nafasi yenye uwezo wa kuathiri sera nje ya mipaka ya Ulaya na hata kufikia Afrika Mashariki. Nafasi hii inajulikana kama Urais wa Baraza la Umoja wa Ulaya.
Katika makala hii nitaeleza na kufafanua maana na umuhimu wa nafasi hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania. Maana Umoja wa Ulaya (EU) ni ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi 27 za Ulaya na Denmark ni miongoni mwao.
Kwa pamoja, tunashughulikia masuala mengi kuanzia biashara, mabadiliko ya tabianchi, usalama na uhamiaji kupitia taasisi na sera za pamoja. Moja ya taasisi hizo muhimu ni Baraza la Umoja wa Ulaya ambalo mara nyingi huitwa Baraza la Mawaziri.
Kila baada ya miezi sita, nchi moja ya Umoja wa Ulaya inashika urais wa baraza hili. Hii ina maana kuwa nchi
hiyo inaongoza mikutano, inaweka ajenda na kusaidia serikali za Umoja wa Ulaya kufikia makubaliano kuhusu
sheria na sera mpya. Kwa sasa ni zamu ya Denmark kushika jukumu hilo ambalo imeanza kulitekeleza kuanzia Julai Mosi, 2025.
Denmark inachukua nafasi hiyo kutoka kwa Poland na jukumu kubwa na muhimu inayolishikilia kwa sasa ni kuhakikisha maelewano, kusimamia sheria na kusukuma mbele vipaumbele muhimu kwa Ulaya na dunia kwa ujumla. Kwetu Denmark, huu ni wajibu mkubwa lakini pia fursa muhimu.
Chini ya kaulimbiu: ‘Ulaya Imara Katika Dunia Inayobadilika,’ urais wetu unalenga kuijenga Ulaya yenye usalama zaidi, ushindani zaidi na inayozingatia mabadiliko ya kijani. Hata hivyo, Ulaya haipo peke yake. Uamuzi unaofanyika Brussels Mji Mkuu wa Umoja wa Ulaya huathiri uwanja mzima wa kimataifa katika biashara, tabianchi, nishati na maendeleo.
Kadiri Afrika inavyozidi kuwa mhimili muhimu katika siasa za dunia, Ulaya inapaswa kuonesha uwezo zaidi kama mshirika si tu kama mfadhili, bali mshirika anayesikiliza, anayejifunza, na anayechukua hatua kwa maslahi ya pamoja. Mshirika anayeheshimu na anayetekeleza kwa matokeo ya kweli.
Tunaishi katika nyakati za sintofahamu. Migogoro, mitikisiko ya kiuchumi na ushindani wa madaraka duniani vinaunda mpangilio mpya wa dunia. Hivyo, amani haiwezi kuchukuliwa kwa wepesi ndiyo maana urais wa Denmark unalenga kuimarisha uwezo wa Ulaya kujilinda, kulinda demokrasia na kupunguza utegemezi kwa washirika wasioaminika.
Lakini usalama wa Ulaya unategemea pia ushirikiano wa kimataifa, Afrika ikiwa ni mshirika muhimu kwa kuwa inakabiliwa na changamoto zinazofanana ikiwemo ya ugaidi, mashambulizi ya kimtandao, masuala ya uhamiaji holela na taarifa potofu.
Tunashirikiana katika misingi ya pamoja kutafuta amani, utulivu, maendeleo ya kiuchumi na heshima kwa watu wetu. Denmark itahakikisha Umoja wa Ulaya unaimarisha ushirikiano wake na Afrika katika maeneo haya kwa msingi wa mazungumzo, vipaumbele vya pamoja na dhamira ya muda mrefu.
Nguzo ya pili ya urais wetu ni ushindani wa kiuchumi unaotegemea hitaji la haraka la mabadiliko ya kijani. Ulaya inapaswa kuwa kinara katika nishati safi, ubunifu wa kidijiti na miundombinu inayokidhi mahitaji ya baadaye. Tunapaswa kufanya hivyo kwa njia inayozalisha ajira, kupunguza urasimu na kuharakisha ukuaji endelevu. Hii pia inafungua milango mipya ya ushirikiano na Afrika.
Mkutano wa kimataifa wa ‘COP30’ kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika hivi karibuni utakuwa fursa muhimu ya kuchukua hatua kwa pamoja duniani. Kwa sasa, Denmark inaongoza uratibu wa ndani wa Umoja wa Ulaya kuhusu mabadiliko ya tabianchi, huku wakati huo huo Tanzania ikiongoza kundi la Afrika la majadiliano kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Mlingano huu unaweka nchi zetu mbili katikati ya mazungumzo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kila mmoja upande tofauti wa meza ya mazungumzo, lakini tukiunganishwa na lengo moja. Ni fursa ya kipekee kwa vipaumbele, kujenga uaminifu, na kusukuma maendeleo ya kweli kwa pamoja.
Hii inajumuisha kukuza biashara yenye usawa, kuongeza fedha kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi na kujenga mifumo ya uwekezaji yenye manufaa kwa pande zote. Mpango wa Umoja wa Ulaya wa Global Gateway unatoa jukwaa moja ambalo Ulaya inaweza kusaidia maendeleo ya miundombinu, nishati na teknolojia barani Afrika.
Denmark itaweka msukumo kuhakikisha mpango huu unakuwa wenye ufanisi, haki na unaozingatia umiliki wa nchi husika. Hii si mara ya kwanza kwa Denmark kushika urais wa Umoja wa Ulaya. Tumeshawahi kuongoza mara kadhaa, ikiwemo mwaka 2002 tulipoongoza upanuzi wa kihistoria wa Umoja wa Ulaya.
Lakini hali sasa ni tofauti. Umoja wa Ulaya wa leo una changamano zaidi na dunia inakabiliwa na hali ya sintofahamu na misukosuko. Urais wa sasa hauhusiani tu na masuala ya ndani, bali pia na nafasi ya Ulaya katika masuala ya kimataifa na ndiyo maana tunachukua jukumu hili kwa uzito mkubwa.
Katika miezi ijayo, Denmark itakuwa mwenyeji wa mikutano ya ngazi ya juu kimataifa, itaongoza michakato muhimu ya kisheria na kusaidia kuamua aina ya Ulaya tunayotaka iwe katika miaka ijayo. Hapa Tanzania, Denmark itaendelea kuunga mkono ujumbe wa Umoja wa Ulaya na kushirikiana na nchi wanachama wake katika juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania.
Tunatumaini urais wetu utakumbukwa kwa kuwa wa ufanisi, wa vitendo na wenye maono, lakini pia kwa kuwa wa mtazamo mpana wa haki na ulio wazi kwa mazungumzo na washirika duniani. Bila shaka tunazungumzia pia washirika wetu wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Katika miezi ijayo, tunatazamia kutumia urais huu kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wetu na taasisi za Kitanzania na kuonesha maslahi ya pamoja yanayoiunganisha Ulaya na Afrika. Ama iwe ni kuhusu mabadiliko ya tabianchi, biashara, uhamiaji au demokrasia, tuna nguvu zaidi tukikabiliana na changamoto hizo kwa pamoja. Denmark iko tayari kuongoza na kusikiliza.
Mwandishi wa makala hii ni Balozi wa Denmark nchini Tanzania.



