‘Usafiri wa uhakika unachochea kasi ukuaji uchumi’

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema huduma za uhakika za usafiri na usafirishaji ni msingi katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.

Amesema sekta ya usafiri na uchukuzi husababisha kulinda mitaji, kushawishi uwekezaji, kuimarisha mawasiliano kwa wafanyabiashara na watoa huduma nyingine pia husaidia kuzalisha ajira, kupunguza umasikini na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na pato la taifa kwa ujumla.

Majaliwa amesema hayo leo Machi 26, 2024 katika mapokezi ya ndege mpya ya abiria aina Boieng 737-9 MAX katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Sekta ya uchukuzi ni muhimu sana katika kuongeza uwezo wa taifa letu kujitegemea kiuchumi,” amesema kiongozi huyo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua sekta ya uchukuzi kwenye ukuaji wa Uchumi, imeendeleza yale yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta hiyo, ili iendelee kuwa injini ya uchumi wa taifa.

“Na hatua hizi zinaridhisha kupitia maboresho yanayofanywa ya mifumo, sheria, sera na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yetu kupitia sekta ndogo ya usafiri wa anga, usafiri wa maziwa, wa bahari pamoja na usafiri wa reli na barabara,” amesema Majaliwa.

Amesema kutokana na jiografia ya nchi ya Tanzania, serikali inaendelea kufanya juhudi za makusudi katika kuimarisha sekta ya uchukuzi na usafirishaji ili kila pembe ya nchi iweze kufikika.

Habari Zifananazo

Back to top button