Usajili 2024: Fadlu Davis anukia Simba

DAR ES SALAAM – UONGOZI wa Simba umekutana na kufanya mazungumzo na Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi na Uhuru, Dar es Salaam.

Fadlu Davids mwenye umri wa miaka 43, ni raia wa Afrika Kusini na kwa sasa ni kocha msaidizi wa Raja Casablanca ya Morocco na inaelezwa Bodi ya Simba jana imekubaliana naye kuwa kocha mkuu kabla ya kuanzia msimu ujao baada ya kikao chao.

Kwa mujibu wa mitandao ya Afrika Kusini, Bodi ya Simba imefurahishwa na Davids kutokana na mafanikio ya timu anayofundisha na wasifu wake kama kocha bora wa kisasa anayeweza kujenga timu mpya.

Wakala ya Fadlu David alithibitisha kutakiwa kwa kocha huyo na kocha mwenzake wa zamani wa Orlando Pirates, lakini akasisitiza kuwa wanaangalia kwanza mchezo wa Raja Casablanca wa fainali za Throne Cup dhidi ya ASFAR ya Nasreddine Nabi.

Fadlu Davids ana Leseni ya Uefa Pro Licence, anapendelea mfumo wa 4-2-3-1. Msimu wa mwaka 2018/19 na 2021/22 alikuwa kocha msaidizi wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, msimu wa 2022/23 alikuwa kocha msaidizi wa Locomotiv Moscow ya Russia, msimu wa 2023/24 alikuwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca ya Morocco hadi sasa.

Davids amekuwa sehemu ya wanaounda benchi la ufundi la Joe Zinnbaeur, raia wa Ujerumani ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Raja Casablanca, mara zote anapoajiriwa kocha wake msaidizi ni Davids. Davids ameshakuwa kocha mkuu mara kadhaa akiwa na kikosi cha Orlando Pirates pamoja na Martizburg United zote za Afrika Kusini.

Simba wanatafuta kocha kuziba nafasi ya kocha Abdelhak Benchikha wa Algeria, akiwa ni kocha wa saba ndani ya miaka minne wakitanguliwa na Sven Vandenbroeck, Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Manojlovic, Robertinho na Dani Cadena tangu 2020.

SOMA: Yusuf Manji kuzikwa leo Florida

Davids aliwahi kuwa mshambuliaji Afrika Kusini na mara ya mwisho alichezea klabu ya Maritzburg United. Mapema mwezi huu Simba inatarajiwa kwenda kuweka kambi nchini Misri katika mji wa Ismailia kwa muda wa wiki nne na wakirudi watakuwa na Tamasha la Simba Day Agosti 3.

Habari Zifananazo

Back to top button