MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk Venance Mwasse, amesema serikali imeleta mageuzi makubwa ndani ya sekta ya madini kwa kuwezesha ushiriki wa wazawa katika uvunaji wa rasilimali hizo.
Dk. Mwasse amebainisha kuwa serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa nje, hali ambayo imepelekea migodi mingi kufanya vizuri na kusababisha utulivu baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo, jambo linaloleta uwiano katika sekta hiyo.
“Mafanikio ya sekta yanapimwa vizuri sana kwa kuangalia ni nini kimefanyika kuwawezesha wachimbaji wazawa, pamoja na taasisi za ndani kushiriki kwenye mnyororo wa kuongeza thamani wa sekta ya madini,” amesema Dk. Mwasse wakati akizungumza katika mdahalo uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuvutia wawekezaji wa kigeni kwa lengo la kukusanya kodi na mapato yasiyo ya kodi, lakini pia imeweka mazingira wezeshi kwa wananchi wake kushiriki katika uvunaji wa rasilimali za madini.
“Sisemi kwamba wawekezaji wa nje wasiruhusiwe, lakini pia ni muhimu kuwawezesha wananchi wa ndani ili kunufaika ipasavyo,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Dk Mwasse ameeleza kuwa serikali imenunua mashine za kuchoronga mahususi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ambazo zinawasaidia kufanya uchimbaji wa uhakika na kuwawezesha kupata mikopo kutoka benki kutokana na uhakika wa rasilimali wanazozalisha.
Kuhusu mafanikio ya Stamico, Dk Mwasse amesema miradi inayotekelezwa na shirika hilo imekuwa sehemu ya kukusanya mapato badala ya kuwa mzigo wa matumizi na kupelekea ongezeko la mapato kutoka Sh bilioni 1.31 hadi kufikia Sh bilioni 86.
“STAMICO ilikuwa karibu na kufutwa, lakini tumefanya mageuzi makubwa, sasa tunajitegemea, hata katika ulipaji wa mishahara, na pia tunatoa gawio kwa serikali,” amebainisha Dk. Mwasse.