Ushirikiano wachimbaji madini kuimarisha soko

WACHIMBAJI wa madini mkoani Kigoma wametakiwa kuunda umoja na ushirikiano na wachimbaji na wanunuzi wa madini kutoka nchi za ukanda wa maziwa makuu ili kuimarisha soko la madini nchini.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini nchini , Mhandisi Yahaya Semamba alisema hayo akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wachimbaji wadogo wa madini na kusema kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi ambayo yanaimarisha ubia kwenye masuala ya madini baina ya Watanzania na watu wanaoshughulika na madini kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa kumarishwa kwa shughuli za utendaji kwa wachimbaji wadogo kumewezesha wachimbaji hao kuongeza makusanyo ya pato la serikali katika sekta ya madini kufikia asilimia 40 na mpango wa serikali ni kuwezesha wachimbaji wadogo kuingiza asilimia 50 ya pato la taifa kutokana na madini ili mapato hayo yawe sambamba na wachimbaji wakubwa.
Ameupongeza Mkoa Kigoma kuongeza mapato ya serikali katika sekta ya madini kwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 1.
3 katika lengo la kukusanya Sh bilioni 1.6 ambapo lengo likiwa serikali kukusanya kiasi cha Sh bilioni 822 kwa mwaka huu wa fedha.
Awali akizungumza kabla kufunguliwa kwa mafunzo hayo Katibu Msaidizi wa Chama cha wachimba madini mkoani Kigoma (KIGOREMA), Boaz Mkohozi alisema kuwa wanashukuru serikali imeanza kurekebisha changamoto zilizopo kwenye sekta ya madini ili kuwezesha wachimbaji na watu wanaoshughulika na madini kazi zao kuwa na tija.
Hata hivyo alisema kuwa bado wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya vifaa duni katika kazi zao sambamba na changamoto ya upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za fedh ili wanunue zana bora na za kisasa.