Usomaji vitabu una raha yake

DAR-ES-SALAAM : KUNA msemo unaosema ukitaka kuwaficha Waafrika  weka kwenye kitabu. Ukichunguza  utagundua msemo huu ulihusisha utafiti ambao waafrika walikuwa hawana mazoea ya kusoma vitabu.

Katika miaka mingi sasa, watu wengi wamekuwa  wakipendelea kuangalia televisheni na mengine kuangalia mitandaoni  ambayo yamewakengeusha  wasisome  vitabu na kubaki kuwa historia.

Mwandishi Jane Healy  alinukuliwa katika kitabu chake cha mwaka 1990, Endangered Minds, aliandika hivi: “Kadiri muda unavyopita huenda watu wakaacha kusoma.”

Miaka  ya nyuma watu walikuwa  hawawezi kuacha kusoma vitabu na wengine kudiriki kusoma hadithi katika vijarida vidogo kama vile jarida la sani ambalo lilikuwa maarufu sana kusomwa na watu wengi wakubwa na wadogo pia na lengo lilikuwa ni kuongeza maarifa.

Lakini sasa, miaka 30 baadaye imepita ambapo wakufunzi  wengi hasa katika nchi ambazo teknolojia imekua na inatumika sana, wamesema wastani wa vijana wengi kwa sasa  hawawezi kusoma kama ilivyokuwa zamani.

Tabia ya kuacha kusoma vitabu imekuja hivi sasa baada ya watu wengi kuona wanapoteza muda mwingi wa kuelewa na kutafakari katika mambo mbalimbali,  wakiwa wanasoma vitabu na wengi wao wanapendelea kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii.

Kuna faida  nyingi za  kusoma  vitabu licha ya kuongeza maarifa, lakini pia kitabu kinaweza  kumbadilisha mtu na mtazamo wake na hata kumjenga katika mambo mablimbali ya maisha.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, licha ya kuwepo majarida, lakini pia kulikuwa na vitabu mbalimbali vya Kiswahili hasa vile vya kipelelezi ambavyo vijana wa wakati huo walikuwa wanajivunia sana kusoma na ukiwa hujasoma wenzako wakihadithia unajiona umepungukiwa kitu.

Ni wakati ambao vitabu kama vya Njama, Kufa na Kupona, Kikomo, Kikosi cha Kisasi vyote vikitungwa na Elvis Musiba, ambaye mhusika wake mkuu alikuwa ni Willy Gamba, mpelelezi wa Kitanzania aliyekuwa anaogopa barani Afrika kama si duniani kwa ujumla.

Vuta picha vitabu ya mtunzi Benny Mtobwa kile kinachoitwa Tutarudi na Roho Zetu, mhusika mkuu akiwa Joram Kiango.  Pia kuna vitabu vya Muhamed Said Abdulla Bwana Msa, baadhi ya vitabu vyake ni Kosa la Bwana Msa, Siri ya Sifuri, Kisiwa cha Giningi, Mke Mmoja Waume Watatu na Mwana wa Yungi Hulewa.

Hakika usomaji wa vitabu una raha yake vipo vitabu vya Shafi Adam Shafi, baadhi ni Kasri Ya Mwinyi Fuad na Kuli ambacho kilikuwa kinatumika kufundishia riwaya watoto wa sekondari miaka ya nyuma.

Vitabu vingine ninavyokumbuka ni Akuanzae Mmalize, Kamlete Akibisha Mlipue, Salamu Toka Kuzimu, Kikomo. Pia kuna vile vya mtunzi Hammie Rajabu, anda ya Jambazi, Roho Mkononi na Simu ya Kifo kuvitaja kwa uchache.

“Willy, Willy Gamba, umesema ndiye wewe! Loo! Siamini masikio yangu ni wewe kweli, kweli! Nimesikia jina lako mara nyingi. Nimesikia sifa zako. Nilikuwa nikidhani ni hadithi tu kama tunazosoma katika vitabu. Sikufikiria ama kuota kama nitakuona. Nimesoma habari zako katika magazeti, lakini nilikuwa sijaota ya kuwa siku moja nitalala kitandani na Willy Gamba,” alisema Lina huku akitetemeka na kunibusu, “Nini kimekuleta sasa hapa, Willy?” aliuliza.

“Nilifikiria sana kama naweza kumwambia. Mwishowe nikakata shauri nimwambie kwani siye nyakati zingine huwa tunaropoka kusudi tuone nini kitatokea.

Mara nyingi huwa tunajitega wenyewe halafu tunatafuta njia ya kujinasua tena. Hivyo nilimweleza mambo yote tangu mwanzo mpaka mwisho.

Pia nilimweleza jinsi tunavyomfikiria Benny. Na jinsi ambavyo tumenusurika usiku wa jana,”hicho ni sehemu ya kipande cha kitabu cha Kufa na Kupona, ambacho mhusika ni Willy Gamba.

Tuachane na Willy Gamba na Joramo Kiango, tumgeukie David Aggrey  ni miongoni mwa vijana walionufaika na usomaji wa vitabu, ambaye sasa ameweza kuandika kitabu cha hadithi za watoto.

“kila muda nasoma vitabu hasa nikiwa  shuleni naenda maktaba, imenisaidia na kuibua kipaji changu cha uandishi wa kitabu”, anasema David na kuongeza:

“Juni mwaka huu nilianza kuandika na kila nilichoandika nilikiwasilisha kwa mwalimu wangu, ambaye alinisaidia kukiboresha na sasa kinaweza kusomeka.”

Anasema miongoni mwa faida nyingine ya usomaji wa vitabu ni kuwajenga watu ama watoto kifikra  au hata kimawazo.

“Kama  jamii tunaiambia ni bora kuwekeza kwenye vitabu ndio maana baadhi ya shule zina maktaba, mule ndani ya maktaba kuna vitabu mbalimbali, hatuwezi kumwambia mtoto asome vitabu vigumu anatakiwa kuanza  na vitabu vya hadithi ndio aweze kuvutiwa  ndio maana shule nyingi zimeanzisha klabu za usomaji wa vitabu na usomaji wa vitabu  zimeanza  kurudi kama zamani,” anasema na kuongeza:

“Ukisoma vitabu kunaongeza ufahamu wa lugha  mbalimbali kwa mtoto na kuongeza  uwezo wa misamiati ya kuwasiliana, kujiamini na kila unachokifanya  kinakupa  ujasiri na uthubutu katika maisha.”

Tabia ya usomaji wa vitabu hapa nchini imeanza  kupungua kadri siku zinavyokwenda na hii inatokana na matumizi ya Tehama ambayo yamewafanya watu kusahau kusoma vitabu.

TAZAMA: MTOTO DAVID, KIPAJI KILICHOJIFICHA KWENYE KITABU

SOMA:  Wanafunzi Geita wapewa vitabu 52,683

Habari Zifananazo

Back to top button