Utafiti, Tehama njia bora kutunza afya kwa jamii
“TANZANIA kwa mara ya kwanza tulishaanza kupandikiza uloto, tumeshapandikiza wagonjwa 11 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na mmoja kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa hiyo vitu vinawezekanika.
”
Ni kauli ya Dk Stella Rwezaula wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Anasisitiza jambo hilo linawezekana, ni vema serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ikawekeza kwa Watanzania katika teknolojia muhimu kama hizo.
Aina hiyo ya matibabu inahusisha uvunaji, uchakataji na upandikizaji wa chembechembe hai mama za damu ambazo hutolewa kwa watu wenye magonjwa ya saratani ya damu na saratani inayohusisha tezi.
Matibabu hayo pia hutolewa kwa wagonjwa wasioweza kuzalisha chembe hai za damu wakiwemo wa selimundu.
Dk Rwezaula anasema teknolojia kama hizo zinawezekana nchini kinachotakiwa ni kuwawezesha wanasayansi wa Tanzania kufanya tafiti hizo kuokoa maisha ya Watanzania.
Anaeleza teknolojia inapokua kwa upande wa viwanda, inasababisha kuibuliwa kwa magonjwa ambayo hayakuwepo zamani.
“Kunakuwa na mabadiliko ya vinasaba ambayo si kawaida na kusababisha kupata magonjwa mapya, ndio maana watu wanakuwa wanasema kuna magonjwa mapya mengi yanatokea mengi yakiwepo ni saratani.
“Siku hizi kuna saratani za kila aina na magonjwa mengi yanaibuka ni lazima sasa tupambane. Magonjwa mengi kama saratani au ya kurithi yanayotokana na mabadiliko ya vinasaba lazima kwenda na tiba za vinasaba,” anasema.
Anasema sasa wanahamia kwenye teknolojia ya kutibu kwa kutumia vinasaba magonjwa ya kurithi ambayo zamani yalidhaniwa hayatibiki kama selimundu, haemophilia na saratani lakini sasa watu wanapona.
Dk Rwezaula anasema bioteknolojia ni teknolojia inayotumia viumbe hai kwa ajili ya kutoa mazao unayotaka au kuweka mifumo ya kufanyia utatuzi wa mambo.
“Mfano ukichukua hamira ukatengenezea maandazi ni baiteknolojia, ukitengeneza pombe ya kienyeji ni bioteknolojia, lakini tumekuwa tukitumia baiteknoloji ya kupandikiza wanyama, unataka upande ng’ombe anayetoa maziwa mengi lakini anastahimili maradhi, unaenda kutafuta dume unapandishia mpaka unapata unachokitaka ni baiteknolojia,” anasema Mhadhiri na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ally Mahadhy.
Anasema imekuja teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) ambayo mtu anaweza kuchukua taarifa anayoitaka kutoka kwa kiumbe ambaye ana sifa anayoitaka kwa kumpa kiumbe ambaye hana.
“Hii teknolojia ya uhandisi jeni si kama hatuitumii, tayari tunazo bidhaa tunazitumia ambazo mazao yake ni uhandisi jeni, kwa mfano insulin ambayo huwa wanachomwa watu wenye sukari ili kupunguza sukari ile asili yake inatoka kwa binadamu na kwa nguruwe.
“Zamani kabla ya uhandisi jeni kuwepo ile insulin ilikuwa inatengenezwa kutoka kwa nguruwe kwa kutumia kongosho zake, umchinje nguruwe uchukue kongosho ukamue usafishe, unatakiwa uwe na wastani wa tani tano za kongosho kwa ajili ya kupata nusu kilo ya insulin.
“Sasa kama kusingekuwa na bioteknolojia sijui tungekuwa tunaua nguruwe wangapi mpaka insulin ya magonjwa ya sukari iwepo kwa kuwa mahitaji ni mengi tani tano za kongosho unachinja nguruwe wengi sana,” anasema Dk Mahadhy.
Kuhusu mchango wa baiteknolojia ya kisasa katika kuendea mapinduzi ya nne ya viwanda, Mhadhiri na mtafiti katika eneo la bioteknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Daniel Maeda anasema kwa magonjwa ya selimundu sasa hivi mgonjwa anatibiwa kwa kufanyiwa uhariri jeni kwenye eneo lenye hitilafu.
Anasema kinachofanyika ni kuondoa hitilafu na kuweka nakala iliyo sawa hivyo mgonjwa anaendelea na maisha. Anasema wapo wagonjwa waliotibiwa.
“Wagonjwa wa sukari wanafahamu tiba ya insulin ambayo inatumika dunia nzima sasa hivi imetokana na baiteknolojia ya kisasa. Miaka ya 1930 ilitoka kwa mbwa, walikusanya kongosho za mbwa walisaga na kuchuja insulin kisha wanawapa watu. Unaweza kufikiria wagonjwa hao wapo wangapi duniani na mbwa wapo wangapi,” anasema Dk Maeda.
Naye Dk Brian Tarimo kutoka Taasisi ya Afya Ifakara, Morogoro anasema ili kukabiliana na mbu anayeambukiza malaria hivi sasa wanatumia teknolojia ya kisasa kumfanya mbu kukosa uwezo wa kusafirisha malaria.
Anasema ugonjwa wa malaria umekuwa ukiua karibu watu 620,000 kwa mwaka japokuwa mbinu za kumtibu zinajulikana lakini bado malaria imekuwepo, hivyo sayansi pekee ndio suluhisho.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka nchini Ethiopia, Daba Tadessa anasema: “Hakuna ubaya wowote katika teknolojia hiyo ya mabadiliko ya kijenetiki, kwani tunatumia teknolojia hiyo kwenye tiba na dawa.
“Katika chakula, huchakatwa na kumeng’enywa na hatimaye kufyonzwa kama protini au aina nyingine za vyakula kutoka chanzo chochote kile hufuata utaratibu huu.”
Mtafiti mwingine kutoka nchini Burkina Faso, Dk Traore Edgar, anaona teknolojia ya uhandisi jeni ni kama teknolojia nyingine ya uboreshaji wa maisha ya binadamu.
Akielezea uzoefu wa Burkina Faso katika teknolojia hiyo ya uhandisi jeni kwenye zao la pamba, anasema wazalishaji binafsi wameiunga mkono na kwa Afrika teknolojia hiyo imeleta mapinduzi ya kilimo katika nchi za Afrika Kusini, Sudan, Burkina Faso na Nigeria.
“Kwa kutumia teknolojia hii mbegu zinaweza kutengeneza kinga yake dhidi ya wadudu hivyo kutoa suluhu kwa njia ya kawaida ambayo ingehitaji nguvu kazi kwa ajili ya kufanya kazi hiyo,” anasema Dk Edgar.
Anasema teknolojia hiyo ina uwezo wa kutengeneza kinga dhidi ya magonjwa ya virusi na virutubisho. “Hata hivyo, GMO bado inaogopeka Afrika kutokana na mijadala pinzani inayoendelea dhidi yake.”
Anashauri Afrika baada ya kuyakosa mapinduzi ya kijani ya kiulimwengu ina nafasi ya kuhodhi teknolojia za kibunifu kama hizi iweze kujitosheleza kwa chakula.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk Deusideth Mbanzibwa, anasema sera za nchi zinaruhusu utafiti kinachotakiwa ni kufuata taratibu zilizowekwa.
Serikali iliandaa na kuweka Sera ya Taifa ya Bioteknolojia ya mwaka 2010, Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 pamoja na Mfumo wa Taifa wa Usimamizi wa Bioteknolojia ya Kisasa wa mwaka 2005 unaojumuisha sera na miongozo ya mazingira na matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa.
Kwa kuzingatia umuhimu huo, Februari 12, mwaka jana Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliagiza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kufanya majaribio ya bioteknolojia.