Utafiti: Ukatili kwa watoto umepungua

DAR ES SALAAM: MTOKEO ya Utafiti mpya wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto na vijana mwaka 2024 yanaonesha kuwa ukatili wa Kingono,kihisia na kimwili kwa watoto umepungua kwa kiasi kikubwa ililinganishwa na utafiti uliofanyika mwaka 2009.
Utafiti huo mpya umeonesha kwa watoto wa kike ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 33 hadi asilimia 11,ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 76 hadi asilimia 24 na ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 25 hadi asilimia 22.
Na kwa watoto wa kiume ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia tano,ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 74 hadi asilimia 21 na ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 16.
Akitoa matokeo ya utafiti huo leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsi,Wanawake na Makundi Maalum,Dk Dorothy Gwajima amesema utafiti ulifanyika kati ya mwezi Machi na Juni, 2024 na uliwafikia zaidi ya watoto 11,414 wenye umri wa miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Matokeo haya yatawezesha Serikali na Wadau kuboresha na kuandaa Mipango, Programu na Mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili nchini itayoimarisha Ulinzi na Usalama wa Watoto na Vijana na Maslahi mapana ya kizazi cha sasa na cha baadae.
Aidha, amesema kupungua kwa vitendo vya ukatili inaonesha mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali na Wadau katika kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na vijana, kwa kuendelea kutoa elimu mbalimbali kwa umma, pamoja na juhudi za wizara.
“Tumeimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13,kutekeleza na kuratibu Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa lengo la kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili.
Dk Gwajima pia amesema wametekeleza Programu ya Kitaifa ya Tanzania ya Kizazi Chenye Usawa,Kutoa huduma kwa Manusura wa Ukatili wa Kijinsia na ukatili dhidi ya watoto,kuratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni na kuratibu afua za kijamii kwa kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vya ukatili,.
Pia amesema wamewezesha wanawake kiuchumi na upatikanaji wa haki, ulinzi, na malezi chanya ya watoto,kuokoa watoto Wanaoshi na Kufanya Kazi Mtaani kwa Kuratibu juhudi za kuwaokoa watoto walioko katika mazingira hatarishi mitaani na kuwapatia huduma stahiki.
” Kuratibu na kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za maendeleo,kuratibu utoaji wa mafunzo kuhusu Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa Maafisa ili kuimarisha usimamizi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Ameeleza kuwa watoa mafunzo kwa waandishi na kutoa huduma katika Vituo 32 vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers) na kushughulikia mashauri ya watoto kwa kutumia mfumo wa usimamizi wa mashauri ya watoto (NICMS – 2017).
Dk Gwajima amesema ukatili huleta athari za muda mrefu za kiafya ikiwa ni pamoja na matatizo ya afya akili, mawazo ya kujiua, tabia hatarishi za ngono, uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya zinaa ikiwemo VVU, matumizi ya dawa za kulevya na kupunguza fursa mbalimbali za kimaendeleo na kuongeza umaskini katika jamii.
“Napenda pia kuwashukuru Serikali ya Marekani ambayo ndiyo imefadhili utafiti huu chini ya Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI kupitia Shirika la CDC,Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Wizara ya Afya,Ofisi ya Rais –TAMISEMI na TPHS.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Zanzibar Khatibu Mwadini amesema serikali ya Zanzibar itahakikisha kuwa itakapohitaji mapitio ya sheria na sera itaweza kutekeleza ipasavyo.
Naye Kaimu balozi wa Marekani,Andrew Lentz amesema minyororo ya ukatili inaendelea kufuatiliwa na kuvunjwa kuhakikisha kila mtoto Tanzania anakua bila ukatili.
“Marekani inajivunia kuwa sehemu ya kutengeneza kesho nzuri ya watoto na Tanzania imeonesha uongozi wenye alama kufanya utafiti huu ambao pia ulifanyika 2009.