HALMASHAURI ya Wilaya ya Bukombe imefanikiwa kupunguza tatizo la utapiamulo uliokithiri kwa wastani wa asilimia 34, kutoka wastani wa watoto 23 kwa mwaka mpaka kufikia watoto 15 kwa mwaka.
Ofisa Lishe Wilaya ya Bukombe, Lissa Mwakyusa amesema hayo wakati akitoa taarifa fupi ya shughuli za lishe kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024.
Lissa amesema hayo ni mafanikio ya kuhamasisha uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula ikiwemo madini ya chuma zinki, asidi ya folki kwenye unga wa mahindi.
Amesema usimamizi thabiti umewekwa kwenye uhamasishaji na utoaji wa elimu ya lishe bora kwa vijana barehe, mama wajawazito, watoto wadogo ambao ndio waathirika wakubwa wa lishe duni.
SOMA: Viashiria utapiamlo vyapungua Kagera
Ameeleza, mwitikio wa wajawazito waliopewa vidonge vya kuongeza wingi wa damu imeongezeka na mpaka sasa ni wajawazito 52, 428 kati ya wajawazito 57,812 sawa na asiimia 97.61 wamepewa vidonge hivo.
Amesema pia halmashauri imeweza kufikia asilimia 147 ya watoto waliopewa matone ya nyongeza za vitamin A ambapo watoto 89,161 wenye umri kati ya miezi 6-59 waifankiwa kati ya watoto 60,588.
SOMA: Washauriwa kula mboga mboga kuepuka udumavu
Ameeleza, ili kupunguza udumavu mpaka sasa ni watoto 45,455 wanaonyonya maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo sawa na asilima 88.2 ya watoto wengine waliochini ya miaka sita.
“Pia mkakati wa utoaji wa vyakula katika shule za msingi na sekondari na mpaka sasa wanafunzi wote 126,462 wa shule za msingi na sekondari wanapata angalau mlo mmoja kwa siku wakiwa shuleni,” amesema.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2024, Godfrey Mnzava alisema changamoto kubwa ya lishe ni uandaaji wa chakula usiozingatia uwiano mzuri wa makundi yote ya chakula na ufanyaji wa mazoezi.
Ameagiza wataalamu wa lishe kwenye halmashauri zote wasikae maofisini bali watoke wakawaambie watanzania namna bora ya kubadili mtindo wa maisha ili kuepukana na utapiamulo, udumavu na uzito uliopitiliza.
Mnzava ameagiza kuimarishwa kwa vikundi vya lishe shuleni ili kuwaandaa vijana ambao watakuwa mabalozi wa lishe bora ngazi ya familia na kuondokana na matatizo ya lishe.