Washauriwa kula mboga mboga kuepuka udumavu
WANANCHI wa Tanzania na Afrika wametakiwa kuzingatia kula mboga mboga ili kuepukana na tatizo la udumavu, uzito uliopitiliza na utapiamlo.
Ushauri huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vegetable Center Afrika (Worldveg) Dk Gabriel Rugalema katika Kongomano la siku mbili la Kimataifa la wanasayansi wa mazao ya mboga mboga na matunda lililoshirikisha wanasanyasi 250 kutoka nchi nane za Bara la Afrika, Ulaya na Asia.
Alisema ulaji wa mboga mboga na matunda Afrika na duniani ni mdogo sana kinyume na matakwa ya wataalamu hivyo ni wakati kwa wanasayansi kujipanga na kutoka na majibu sahihi ya hakikisha hali hiyo inabadilika ili ulaji mboga mboga na matunda uweze kukua siku hadi siku kwa ajili ya afya ya mwanadamu na kipato.
Mkurugenzi huyo alisema na kutoa mfano wa Bara la Afrika na kusema kuwa watu wa bara hilo asilimia kubwa wanakula nyama robo na ugali na kufanya mwanadamu kuwa na wanga mwingi mwili na hiyo ni mbaya kiafya hivyo ni wakati wa Afrika kubadilika na kula mboga mboga na matunda kuepuka magonjwa ya udumavu ,utapiamlo na uzito uliopitiliza.
Alisema wanasayansi wanakutana jijini Arusha na kujadiliana kwa kina nini kifanyike ili ulaji wa mboga mboga na matunda uweze kupendwa Afrika na duniani na lengo kuu ni kulinda afya na kuendeleza kipato kwa wananchi wote duniani.
‘’Hili kongamano ni muhimu sana kwa Bara la Afrika kwani wanasayansi wanahimiza kuacha kula hovyo kuepuka magonjwa ya sukari na shinikizo la damu{BP} na kuhimiza ulaji wa mboga mboga na matunda kwa ajili ya afya na kipato’’ alisema Rugalema
Naye Professa wa Lishe wa Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro,Joyce Kinabo alisema kuwa wakati umefika kwa chakula cha mboga mboga na matunda kuliwa shuleni hususani katika shule za bweni za msingi na sekondari kwani ulaji mashuleni wa chakula hicho ni mdogo sana.
Professa Kinabo alisema mtoto wa miezi sita anapaswa kulishwa mboga mboga na matunda kwani hiyo inamsaidia kiafya na kiakili kuliko kumlisha nyama na ugali kumnajazia wanga mwili na ni mbaya kiafya kuliko watu wanavyofikiria.
Alisema wakati imefika kwa wadau wa sekta ya mboga mboga na matunda kwenda mashuleni kote nchini kutoa elimu na kuhimiza ulaji wa mboga mboga na matunda kwa wanafunzi wetu ili jamii hiyo iweze kupenda chakula hicho toka wakiwa wadogo tofauti na sasa mtoto anaona chakula hicho sio muhimu kwa afya.
‘’Katika Kongamano hili tumekutaka wanasayansi na wadau wa sekta ya mboga mboga na matunda kujadili namna gani nzuri ya kuboresha ulaji wa chakula hicho ili kiweze kupendwa na watu wengi duniani tofauti na sasa kwani ni asilimia dogo sana inakula chakula hicho’’alisema Professa Kinabo
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao na Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Kilimo, Dk Nyamizi Bundala alisema asilimia 90 ya watanzania hawali chakula aina ya mboga mboga na matunda hivyo wakati umefika kwa watanzania kula chakula hicho kwa ajili ya afya na kipato.