Teknolojia matundu madogo yaleta mapinduzi matibabu ya uzazi

DAR ES SALAAM: TEKNOLOJIA ya kisasa ya upasuaji wa matundu madogo imeanza kuleta mapinduzi katika matibabu ya matatizo ya uzazi nchini, huku ikisaidia kuziba pengo kati ya mahitaji ya huduma za uzazi saidizi na uwezo mdogo uliokuwepo awali.

Mkurugenzi wa Kituo cha Uzazi cha Nu Life Fertility, Ratheen Rawal, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu mafanikio ya kituo hicho ndani ya kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake.

Rawal alisema mafanikio hayo yanatokana na matumizi ya teknolojia ya urutubishaji nje ya mwili (IVF) pamoja na upasuaji wa kisasa wa laparoscopy, unaofahamika zaidi kama upasuaji wa matundu madogo.

Alieleza kuwa teknolojia hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kushughulikia matatizo ya msingi yanayosababisha utasa, ikiwamo uvimbe kwenye mfuko wa uzazi na ugonjwa wa endometriosis.

Kwa mujibu wake, mbinu hiyo huruhusu matibabu sahihi yenye majeraha madogo, hivyo kutoa suluhisho jumuishi zaidi kwa wagonjwa wa utasa. Hatua hiyo imewezesha watoto 400 kuzaliwa kupitia huduma za kituo hicho ndani ya miaka minne na nusu iliyopita.

 

“Sasa tunaona wagonjwa waliokuwa wamejaribu IVF nje ya nchi bila mafanikio wakirejea na kufanikiwa hapa, hasa kutokana na kuwa tunatoa huduma kamili kuanzia uchunguzi, upasuaji wa matundu madogo hadi IVF ya kisasa chini ya paa moja,” alisema Rawal.

Aliongeza kuwa upatikanaji wa huduma hizo nchini unapunguza gharama kwa wagonjwa kwa kuondoa ulazima wa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.

Aidha, alisema wagonjwa wengi huruhusiwa kurejea nyumbani ndani ya saa 24 baada ya upasuaji na kupona kikamilifu ndani ya chini ya wiki moja, tofauti na wiki kadhaa zinazoweza kuhitajika baada ya upasuaji wa kawaida wa kufungua tumbo.

Rawal alisema upanuzi wa huduma hizo umefanyika wakati viwango vya uzazi vikipungua na uelewa kuhusu teknolojia za uzazi saidizi ukiwa bado mdogo, licha ya mahitaji kuendelea kuongezeka.

Alisema pia serikali imeanza kuunga mkono maendeleo hayo kupitia sera na mageuzi katika sekta ya afya. Alitolea mfano mwaka 2023, serikali ilishirikiana na wadau kuandaa mfumo wa udhibiti wa teknolojia za uzazi saidizi ili kuboresha ubora wa huduma, gharama nafuu na usimamizi wake.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Nayana Patel, alisema kuunganishwa kwa mbinu za kisasa za IVF na upasuaji usiohitaji kufungua mwili ni hatua muhimu katika kuboresha matokeo ya matibabu nchini.

Alisema ingawa IVF imekuwepo duniani kwa zaidi ya miongo minne, teknolojia hiyo imeendelea kupiga hatua kubwa.

“Kilichokuwa kinakosekana katika eneo hili ni upatikanaji wa maendeleo haya, hasa yanapochanganywa na mbinu za kisasa za upasuaji zinazoongeza uwezekano wa mafanikio,” alisema Dk Patel.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button