JUMANNE iliyopita makala haya ya Mwandishi Wetu yalijikita katika Tathmini ya mikataba kuepuka ulipaji kodi maradufu (DTAs) Tanzania.
Mikataba hii ni makubaliano kati ya nchi mbili au zaidi yanayolenga kuepuka kutozwa kodi mara mbili kwa mapato yanayopatikana katika nchi hizo. Leo makala yanajikita kutazama utata au changamoto katika mikataba hiyo.
ENDELEA…
MIKATABA ya kuepuka ulipaji kodi maradufu Tanzania (DTAs) ina nafasi muhimu kusaidia ufi kiaji wa malengo ya maboresho ya kodi nchini kwa kuweka mazingira rafi ki ya kodi kwa wawekezaji.
Kwa kupunguza kutokuwapo kwa uhakika kuhusu kodi kunakotajwa kama kikwazo katika uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI), mikataba hii inajenga imani kwa wawekezaji wa kimataifa.
Kimsingi, mikataba hiyo (DTAs) huondoa hatari ya utozwaji kodi maradufu na kujenga mazingira ya kodi yanayotabirika, yaliyo wazi na yanayowiana na juhudi za Tanzania kufanya mfumo wake wa kodi kuwa wa kisasa na kuimarisha utekelezaji wa taratibu, kanuni na sheria za kodi.
Hata hivyo, kwa kadri sera za kodi za ndani nchini zinavyobadilika, kudumisha uwiano kati ya majukumu ya mkataba na vipaumbele vya kitaifa kunaleta changamoto. Jumanne iliyopita, tuliangalia nafasi DTAs katika kuunda
mazingira ya kodi na kuvutia uwekezaji kutoka nje.
Leo tunajikita katika mijadala na maoni ya wadau kuhusu ugumu na changamoto zilizopo katika utekelezaji zikiwemo za kiutawala, upotevu wa mapato na umuhimu wa kuboresha mikataba wa mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na udhibiti.
SOMA: Tathmini ya mikataba kuepuka ulipaji kodi maradufu Tanzania
Masuala ya utekelezaji Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uhandisi na mshauri wa zamani wa masuala kodi,
Emmanuel Edwin anasema utekelezaji bora wa mikataba ya kuepusha utozaji kodi maradufu Tanzania unakabiliwa na vikwazo kadhaa vinavyopunguza manufaa tarajiwa.
Anabainisha changamoto za kiutawala zikiwamo za ucheleweshaji wa utekelezaji wa mkataba na kukosekana kwa msimamo katika tafsiri za vifungu vya mkataba hali inayosababisha sintofahamu kwa wawekezaji.
“Mambo haya yanachangiwa pia na uhaba wa mafunzo ya kutosha katika mamlaka za kodi hali inayosababisha kuwapo matumizi yasiyofanana ya mkataba huo katika masuala tofautitofauti,” anaeleza.
Anaongeza: “Kutofautiana huko si tu kwamba kunaongeza gharama, bali pia kunahatarisha na kupunguza imani ya wawekezaji katika haki na kutabirika kwa mfumo wa kodi wa Tanzania”.
Anatoa mfano wa utekelezaji wa mkataba wa kuepuka utozaji kodi maradufu (DTA) wa Tanzania na India kama mfano wa changamoto zinazowakabili wawekezaji. Anatumia mfano wa Kampuni ya Bharti Airtel ambayo ni
mwekezaji maarufu wa India katika sekta ya mawasiliano ya simu nchini Tanzania kueleza wasiwasi wake.
Kwa mujibu wa Edwin, marekebisho yaliyofanyiwa mwaka 2013 katika mkataba wa kuepuka utozaji kodi maradufu
(DTA) yakilenga kupunguza utozaji kodi maradufu kwa kutoa mikopo ya kodi kwa kodi zinazolipwa Tanzania,
hayakufanikiwa kutokana na ucheleweshaji mkubwa wa kufanya marejesho na mikopo ya kodi nchini India.
Alihusisha mambo hayo na kukosekana kwa ufanisi wa kiutawala na uratibu duni baina ya mamlaka ya kodi za nchi
zote mbili. Anasema uzoefu kama huo husisitiza kuwapo changamoto za kiutendaji katika utekelezaji wa DTA na hitaji muhimu la kurahisisha michakato ya kiutawala na ushirikiano baina ya nchi mbili.
Kimsingi, mizozo kati ya masharti ya DTA na sheria za kodi za ndani huleta vikwazo vikubwa. Katika hali ambayo mikataba inatofautiana na kanuni za kodi za ndani, mara nyingi utata hutokea na kusababisha mizozo na mazungumzo ya muda mrefu kati ya wawekezaji na mamlaka ya kodi.
Kwa mfano, kukosekana kwa uwiano wazi wa mapato au haki za kikodi kunaweza kusababisha kutozwa kodi maradufu au kutozwa kodi kidogo, na hivyo kuharibu malengo ya DTAs. Ili kuondokana na changamoto hizi, lazima Tanzania ihusishe taratibu za utawala, iwekeze kuwajengea katika kuwajengea uwezo maofisa wa kodi na kuweka miongozo ya wazi zaidi ya kuoanisha DTA na mifumo ya kodi ya ndani.
Matokeo hasi yasiyotarajiwa Mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara (MBA) ambaye ni
mtaalamu wa fedha mwenye uzoefu na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya udalali wa bima inayofanya kazi nchini,
Fred Msangi anaonesha wasiwasi wake kuhusu DTAs.
Anasema, “Ingawa DTAs zimeundwa kuzuia kutoza kodi maradufu, zinaweza pia kuwezesha kuwapo ukwepaji kodi bila kukusudia na ubadilishaji wa faida kwa mashirika ya kimataifa.” Vitendo vya kinyonyaji kama vile ununuzi wa mikataba ambako kampuni hupanga shughuli ili kufaidi masharti ya mkataba yanayofaa zaidi au kutoweka kwa vyanzo (wa msingi na ubadilishaji wa faida (BEPS), ni matokeo ya kawaida yasiyotarajiwa.
Mazoea na taratibu hizi hupunguza mapato ya kodi ya Tanzania na kudhoofisha uwezo wa nchi kufadhili huduma muhimu za umma na miradi ya maendeleo. Kwa mantiki hiyo, mashirika ya kimataifa yanaweza kutumia mikakati ya uhawilishaji bei kuhamishia faida katika maeneo yenye kodi ndogo hata inapotokea shughuli halisi ya kiuchumi nchini.
Tabia hii si tu kwamba inainyima nchi sehemu ya haki yake ya mapato ya kodi, bali pia inazidisha ukosefu wa usawa katika mzigo wa kodi na kuweka mzigo zaidi katika biashara za ndani.
Msangi anasema, “Kukabili hatari hizi, lazima Tanzania ichukue hatua madhubuti kupambana na ukiukwaji huo wa hatua zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka ya manufaa ya mkataba kwa shughuli halisi za kiuchumi, kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa mipakani na kushiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa kama vile mfumo wa BEPS wa OECD.”
BEPS (‘Base Erosion and Profit Shifting’) ni mkakati wa kupanga kodi ambao kampuni za kimataifa hutumia kuhamisha faida hadi maeneo ya chini au yasiyotozwa kodi wakati OECD (‘Organization for Economic Cooperation and Development’) ni shirika la kimataifa linachochea ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo endelevu.
Msangi alisisitiza zaidi mzozo wa kodi wa Mgodi wa Acacia kama mfano wa hatari zinazohusiana na shughuli za
kimataifa nchini Tanzania. Mwaka wa 2017, Tanzania iliituhumu Kampuni ya Madini ya Acacia kwa kujihusisha na mikakati ya kupanga kodi ikiwa ni pamoja na upangaji wa bei na ubadilishaji wa faida, ili kutoa taarifa ya kuwapo
mapato duni na kukwepa kodi.
Kwa mujibu wa serikali, Acacia iliuza madini ya dhahabu nje ya nchi yenye thamani ya Dola bilioni 190 katika kipindi cha miaka 17 huku ikipunguza kwa kiasi kikubwa thamani ya mauzo hayo katika vitabu vyake/ripoti zake.
Licha ya mgogoro huo kutofungamana moja kwa moja na DTA, Msangi anasema ulionesha udhaifu katika mfumo wa
kodi wa Tanzania kwa kuwa ulikuwa unaweza kutumiwa kupitia ununuzi wa mikataba.
“DTA za Tanzania na nchi nyingine kama Canada na Uingereza, ambako kampuni mama ya Acacia ya Barrick Gold inafanya kazi, zinaweza kuwa zimewezesha matumizi ya masharti ya mkataba wa kupunguza mapato yanayotozwa kodi nchini Tanzania,”anasema.
Faida zinazotokana na shughuli za Tanzania zinaweza kuongezwa kupitia mamlaka zenye mikataba ya faida ya kodi na hivyo kumomonyoa wigo wa vyanzo vya kodi. Kuhusu suala Acacia, Msangi anapongeza juhudi za Serikali ya Tanzania kutekeleza kanuni za uwekaji bei za uhawilishaji na kujadili upya mikataba ya uchimbaji madini ili kuziba mianya.
Anasisitiza, “Suala hili linadhihirisha haja ya mikataba ya kuepusha kodi maradufu kujumuisha vifungu madhubuti
vya kupinga ukiukaji, kuzuia unyonyaji wa mikataba na kuhakikisha Tanzania inabaki na mgao wake halali wa mapato kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika ndani ya mipaka yake”.
Utegemezi wa kiuchumi
Mtaalamu maarufu wa masuala ya kodi, Barita Taseni na wadau wengine wa tasnia ya kodi wanasisitiza kuwa licha ya DTAs kuwa na mchango mkubwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) kuja Tanzania, pia zimeibua wasiwasi kuhusu kukuza utegemezi wa kiuchumi kwenye mitaji ya nje kwa gharama ya ukuaji wa sekta ya ndani.
Wanasema uwekezaji wa kigeni ambao mara nyingi husaidiwa na huduma nzuri za kodi chini ya DTAs, unaweza
‘kufunika’ maendeleo ya biashara za ndani. “Biashara za ndani hasa biashara ndogo na za kati (SMEs) mara nyingi hupambana kushindana na kampuni za kigeni zenye mitaji mikubwa zikinufaika na faida za kodi zinazotolewa na DTAs,” anasema.
Mradi wa Bandari ya Bagamoyo unatajwa kama mfano bora wa namna DTA na uwekezaji kutoka nje unavyoweza kusababisha utegemezi wa kiuchumi. Mradi wa Dola za Marekani bilioni 10 unaotarajiwa kuwa moja ya bandari kubwa zaidi barani Afrika, uliongozwa na wawekezaji wa China na Oman chini ya mfumo wa DTA wa Tanzania na mataifa haya.
Licha ya ahadi ya kuingiza mtaji mkubwa wa kigeni, mradi huo uliibua wasiwasi kuhusu athari zake kiuchumi hususani katika viwanda vya ndani na uendelevu wa kifedha wa Tanzania.
Taseni na wakosoaji wengine wanasema masharti ya uwekezaji yalitoa misamaha mikubwa ya kodi na mikataba ya ukodishaji wa muda mrefu kwa mashirika ya kigeni yanaweza kudhoofisha vyanzo vya mapato ya ndani na kuhatarisha mamlaka yake juu ya mali muhimu ya miundombinu.
“Utegemezi wa utaalamu na mtaji wa kigeni unamaanisha ushiriki mdogo wa wafanyabiashara wa ndani na wafanyakazi katika maendeleo na uendeshaji wa mradi hali inayoweka kando michango ya ndani kiuchumi,” anasema Taseni.
Mwaka 2019, Rais John Magufuli alisimamisha mradi huo huku akitaja masharti yasiyofaa yaliyonufaisha wawekezaji wa kigeni kwa gharama ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Taseni, uamuzi huu ulisisitiza hatari za kutegemea zaidi uwekezaji wa kigeni unaowezeshwa na DTAs na kuhimiza umuhimu wa sera zinazotoa vipaumbele uongezaji thamani wa ndani, uhamishaji wa teknolojia na ushirikiano na viwanda vya ndani.
Taseni na wenzake wanasema utegemezi wa uwekezaji kutoka nje unaweka uchumi wa Tanzania katika katika hatari kama mabadiliko ya soko la kimataifa, mabadiliko ya kijiografia na mabadiliko ya vipaumbele vya wawekezaji.
Wanasisitiza haja ya kuwapo sera zinazolenga kuendeleza viwanda vya ndani, kujenga mnyororo wa thamani ya ndani sambamba na kukuza ujasiriamali.
“Ili kupunguza hatari hizi, Tanzania haina budi kuweka kipaumbele katika uhamishaji wa teknolojia, kujenga
uwezo, na kufanya ubia kati ya wawekezaji wa kigeni na wafanyabiashara wa ndani,” anasema Taseni.
Anaongeza: “Kuanzisha sera za viwanda zinazochochea uongezaji thamani wa ndani ni muhimu ili kujenga uhimilivu
na uwiano wa kiuchumi”.
Uchambuzi linganishi
Mmoja wa maprofesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kodi na sheria
za kimataifa za kodi (hataki kutajwa), anasema mbinu ya Tanzania katika mikataba ya kuepuka ulipaji kodi maradufu (DTAs), inaonesha kuwapo mfanano na tofauti ikilinganishwa na nchi jirani na mataifa mengine katika muktadha sawa wa kiuchumi.
Anasema kuchambua mikakati iliyotumiwa na nchi kama Kenya, Uganda na Rwanda katika Afrika Mashariki pamoja na Zambia na Ghana kunatoa uelrwa kuhusu thamani katika kutumia DTAs kuchochea ukuaji wa uchumi na kudumisha usawa na vipaumbele vya ndani vya kifedha.
Anatoa ufafanuzi huo kuhusu mbinu ya Tanzania ya DTAs akitoa uchambuzi linganishi na nchi jirani. “Kenya ina mtandao mpana zaidi wa DTA kuliko Tanzania, ikiwa na makubaliano na zaidi ya nchi 20 kwa uelewa wangu, ikiwa na washirika wakuu kama China, India, na Ujerumani,” anasema profesa huyo.
Anaongeza: “Mara nyingi DTA za Kenya hujumuisha masharti ya kupinga matumizi mabaya kama vile vizuizi vya
manufaa ya mkataba yanayolenga kuzuia ununuzi wa mikataba na ubadilishaji wa faida unaofanywa na mashirika ya kimataifa. Utekelezaji wake wa mpango kazi wa OECD wa BEPS unaonesha mbinu madhubuti za kushughulikia
changamoto za kodi duniani.
Wakati ikipanua mtandao wake wa DTA, Tanzania haijachukua hatua za kina dhidi ya ukiukaji kama Kenya. Hali
hii inaifanya iwe katika hatari zaidi ya mikataba ya kinyonyaji na upotevu wa mapato. Aidha, profesa huyo
anabainisha mtazamo wa Uganda akisema Uganda ina DTAs chache kuliko Tanzania, lakini inatilia mkazo uoanishaji wa masharti ya mkataba na vipaumbele vya kodi ya ndani.
Kwa mfano, Uganda imefanya majadiliano upya kuhusu mikataba kadhaa kujumuisha viwango vya chini vya kodi vya mrabaha na riba kuhakikisha mgao mzuri wa mapato kutokana na uwekezaji wa kigeni.
“Ubia wake na mashirika ya kimataifa kama IMF (Shirika la Kimataifa la Fedha) umesaidia kurahisisha michakato ya mkataba wa kodi. Mtazamo huu wa kujadiliana upya unaipatia Tanzania mwongozo wa kuweka DTAs sawa kadiri hali za kiuchumi zinavyobadilika,” anasema.
Profesa pia anaangazia mikakati ya Ghana kama nchi nyingine yenye rasilimali nyingi. Anasema, “Ghana hutumia DTAs kimkakati kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, hasa katika madini na nishati. Mikataba yake inasisitiza uwazi na kuingiza taratibu thabiti za ubadilishanaji taarifa miongoni mwa mamlaka za kodi”.
Utekelezaji wa kodi wa Ghana kupitia mbinu bora za kimataifa kama vile kujiunga na Mfumo Jumuishi wa BEPS,
umeimarisha uwezo wake kushughulikia mipango ya kukabili ukwepaji kodi. Hii hutumika kama mfano muhimu
kwa Tanzania kuimarisha utekelezaji na kuboresha ufanisi wa mkataba.
Kuhusu Rwanda, profesa huyo anabainisha mtazamo wake mahususi wa kisekta akisema, “Rwanda imefanya
mazungumzo ya kimkakati ya DTAs kwa kuzingatia sekta zinazowiana na malengo ya maendeleo ya kitaifa kama vile
teknolojia na huduma.”
Kwa msingi huo, DTA yake na Mauritius inahusisha masharti katika utatuzi wa migogoro na kuimarisha imani ya wawekezaji. “Tanzania haina budi kujifunza kutokana na mwelekeo wa kisekta wa Rwanda kwa kurekebisha DTAs zake ikilenga sekta zinazokua kama viwanda, kilimo na nishati nishati,” anasema.
Maoni hayo ya profesa yanaonesha umuhimu wa kutumia mikakati iliyoundwa kuongeza manufaa ya DTAs huku ikipunguza vihatarishi vya kinyonyaji na upotevu wa mapato.
Hitimisho
Kuimarisha mikataba ili kuepuka ulipaji kodi maradufu (DTAs) kunahitaji mbinu za kimkakati na uwiano zinazovutia uwekezaji kutoka nje huku zikilinda maslahi ya mapato ya taifa.
Vipaumbele muhimu ni pamoja na kujumuisha vifungu thabiti vya kupambana na ukiukaji kuzuia unyonyaji wa mikataba, kujadili upya mikataba iliyopitwa na wakati ili iendana na vipaumbele vya kiuchumi na kuimarisha uwezo
wa kiutawala ili kuhakikisha kuna ufanisi katika utekelezwaji.
Katika hili, utungaji sera unaojikita katikaushahidi ni muhimu. Hili linahitaji utafiti wa kina kuhusu athari za DTAs
kiuchumi, kiutawala na kisekta ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayopaswa kuboreshwa.
Kwa kutumia mbinu ya kufikiria mbele na kuongozwa na data, Tanzania inaweza kuboresha mfumo wake wa DTA
kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi pamoja na kuendana na maboresho ya kodi na malengo ya maendeleo ya nchi.