Utekelezaji ilani CCM wapaisha uchumi, wakuza pato la taifa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 umeimarisha uchumi na kuongeza ukuaji wa pato la taifa kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi asilimia 5.4 sasa.

Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alipowasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Dodoma.

Dk Biteko alisema katika kipindi cha utekelezaji wa ilani, serikali imeimarisha uwekezaji katika uchumi, maji, afya, elimu na usafirishajina kusaidia kufikia kasi hiyo ya ukuaji wa pato la taifa.

“Kiwango halisi cha ukuaji wa pato la taifa kimeongezeka kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi asilimia 5.4 kwa sasa. Pato halisi la taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 5.4 kutoka ukuaji wa pato la asilimia 5.1 kwa mwaka 2023,” alieleza Dk Biteko.

Alisema pato la wastani la mtu mmojammoja limeendelea kuongezekja kutoka Sh milioni 2,653,790, 2020 hadi Sh milioni 3,055,606 sasa.

“Mapato ya ndani yamefikia asilimia 15.8 ya pato la taifa kwa mwaka 2024/2025, ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 5.5 mwaka 2023/2024 na mapato ya kodi kufikia asilimia 12.9 ya pato la taifa 2024/2025 kutoka matarajio ya asilimia 12.6 mwaka 2023/2024,” alifafanua.

Aliongeza ajira 8,884,204 zimezalishwa kupitia sekta ya umma na binafsi ikiwa ni asilimia 101.05 ya lengo la kuzalisha ajira milioni nane.

Vilevile, Dk Biteko alisema serikali imeimarisha huduma za afya nchini kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 8783 mwaka 2020 hadi vituo 12,846 mwaka huu likiwa ni ongezeko la vituo 4063.

Kwa upande wa sekta ya elimu, alisema bajeti ya elimu imeongezeka kutoka Sh bilioni 312.058 mwaka 2020 hadi Sh bilioni 796.385 mwaka 2025 na wanafunzi wanaonufaika imeongezeka kutoka 14, 940, 2020 hadi 16,155,281 mwaka 2025.

Pia, alisema huduma ya maji imeimarishwa ambapo miradi ya maji 2,331 imekamilika huku miradi 1,965 ikiwa ya vijijini na 366 ni ya mijini na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 83 Desemba 2024.

Katika sekta ya kilimo, Dk Biteko alisema serikali imetekeleza miradi iliyolenga kuleta tija katika uzalishaji wa mazao, kuboresha vyama vya ushirika, miundombinu ya umwagiliaji na upatikanaji wa pembejeo.

“Serikali imepata mafanikio makubwa ya kuimarisha mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani ambapo vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka 2150 mwaka 2020 hadi 4060 mwaka 2024,” alisema.

Alisema mafanikio yaliyopatikana tangu Mei, 2024 hadi sasa katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya kuingia mikataba na Kampuni ya DP World ni pamoja na kuhudumiwa kwa tani zaidi ya milioni 5 ambayo ni zaidi ya asilimia 15 ya shehena tani milioni 4.4 iliyohudumiwa kwa kipindi kama hiki mwaka uliopita.

“Katika kipindi cha Julai mwaka 2024, hadi Februari mwaka 2025 Sh Trilioni 8.26 zimekusanywa sawa na ongezeko la Sh trilioni 1.2 ikilinganishwa na trilioni 7.1 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024,” alieleza.

Aliongeza mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 700 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 3.3 mwaka 2024.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button