Utekelezaji ilani ya 2020/25 ni turufu CCM

KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani Oktoba mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinasema utekelezaji wa ilani na maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni turufu kubwa kwake katika uchaguzi huo.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla anasema hayo kwa nyakati tofauti katika ziara zake za kichama katika maeneo mbalimbali nchini kuzungumza na wanaCCM kuimarisha uhai wa chama.

Akizungumza katika mikutano tofauti ya hadhara, Makalla anasema CCM inamuona na kumtambua Rais Samia kuwa ni karata muhimu katika uchaguzi huo. Anasema kwa kazi alizozifanya Rais Samia, anaingia katika historia kuwa kiongozi aliyeongoza kwa kupeleka fedha za maendeleo zinazoacha alama zitakazokipa nguvu chama chao baadaye.

Anasisitiza kuwa, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kielelezo na ya kimkakati iliyokuwa ndani ya ilani yao, unawapa nguvu ya kutosha katika uchaguzi kwani hawatahitaji kueleza yaliyofanyika kwa kuwa yanaonekana wazi.

Miradi iliyotekelezwa na chama hicho katika kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano imegusa sekta mbalimbali na leo makala hii inajikita katika utekezaji ulifanyika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja kurahisisha shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mbeya
Akiwa mkoani Mbeya, Makalla anaeleza kuhusu ujenzi wa barabara nne katika mkoa huo akieleza umuhimu wa mkoa huo kuwa na barabara zenye kiwango na imara kutokana na kuwa moja ya mikoa muhimu ambayo barabara yake inarahisisha usafirishaji kufikia nchi jirani na mipaka ya Tanzania.

Anasema amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa huo na suala la barabara nne lilikuwa likiongelewa kila kukicha, lakini serikali chini ya Rais Samia imetoa Sh bilioni 138 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya njia nne katika mkoa huo.

Anasisitiza kuwa mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 15.6 kuanza utekelezaji wa mradi huo wa barabara na wanaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara wa zaidi ya kilometa 23 ambazo ujenzi wake unagharimu zaidi ya Sh bilioni 28.

Lindi
Akiwa mkoani Lindi Makalla anasema katika Wilaya ya Liwale mkoani humo wananchi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya barabara, wanyamapori pamoja na umeme vinavyosababisha kukwama kwa shughuli za kiuchumi katika wilaya hiyo.

Katika kufafanua suluhu ya changamoto ya barabara kwa hadhira aliyozungumza nayo, Makalla anawasiliana na waziri mwenye dhamana ya ujenzi, Abdallah Ulega ambaye anakiri kuwa kati ya mikoa yenye changamoto za barabara, Lindi imo na anaahidi kutembelea Liwale na maeneo mengine kuona changamoto hizo na kutafuta suluhu yake.

Akizungumza kwa simu Ulega anaongeza kuwa barabara hiyo ni moja ya sehemu zilizotajwa katika bajeti ya wizara yake kuanzia Nangulukulu mpaka Liwale na kutoka Liwale hadi Nachingwea itakayokuwa na kilometa 50 za kuwekwa lami kutokana na maagizo ya Rais Samia.

“Hii barabara inayokwenda Nachingwea inawaunganisha majirani zao wa Nachingwea mpaka Masasi lakini tutawapa kipaumbele watu wa Liwale kwa sababu upande wao ndo kwenye uzalishaji mkubwa wa korosho zinazotakiwa kufika sokoni,” anasema Ulega.

Anasema serikali imetoa zaidi Sh bilioni 100 kujenga na kuboresha madaraja 10 imara na ya kudumu na makaravati matatu yaliyopo katika barabara ya Kusini kutatua changamoto inayowakuta wananchi hao katika kipindi cha mvua.

Moja ya madaraja hayo ni Daraja la Somanga Mtama lenye urefu wa meta 60 ambalo ujenzi wake unahusisha nguzo 43 zenye urefu meta 12 kwenda chini kila moja ili kuinua daraja hilo.

Mtwara
Makalla anasema Rais Samia amedhamiria kuifungua mikoa ya Kusini kiuchumi kwa kutenga kiasi cha Sh bilioni  234 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kiuchumi yenye umbali wa kilometa 210 kutoka Newala, Tandahimba hadi Masasi ambayo inakwenda kuunganisha Mtwara na maeneo mengine ya Mchuchuma na Mbamba Bay.

Akizungumza kuhusu barabara hiyo Makalla anasema Rais Samia amemtuma apite kukagua barabara hiyo ambayo imetajwa kuwa ya kiuchumi na kueleza kuwa kilometa 50 tayari zimekamilika na alijiridhisha kuwa ujenzi bado unaendelea kufanyika kwani amewakuta wakandarasi wakiendelea na kazi.

Morogoro
Akiwa mkoani Morogoro, Makalla anasema anatambua kuna changamoto za barabara ya kutoka Kilombero hadi Mahenge na ameshafanya mawasiliano na Waziri Ulega ili kutatua changamoto hiyo akiwa kama msaidizi wa rais kwenye ujenzi wa barabara.

Sambamba na hayo Mbunge wa Jimbo la Kilosa Profesa Palamagamba Kabudi anaeleza katika miaka minne ya Rais Samia amefanya mabadiliko katika maeneo mengi ambayo yalikuwa yamesahaulika na kuanza kutaja maendeleo yaliyofanyika kijiji kwa kijiji katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Profesa Kabudi anasema zaidi ya Sh bilioni 1.8 zimetolewa katika Kijiji cha Kijichi kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye umbali wa kilometa 242 kutoka katika kijiji hicho hadi Kijiji cha Luwemba sambamba na barabara ya Kijiji Lumbiji iliyokuwa haipitiki.

Kanda ya Ziwa
Katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Shinyanga Makala anasema Rais Samia amemuenzi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Pombe Magufuli kwa kukamilisha miradi yote ya kimkakati aliyoiacha ikiwemo Daraja la J.P. Magufuli (Kigongo-Busisi) ambalo amelizindua Juni 19, mwaka huu akitaja sifa za daraja hilo kuwa ni daraja la tano kwa urefu Afrika.

Makalla anasema Rais Samia amekwenda mbali zaidi kwa kuendeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Treni ya Umeme (SGR) ambayo inatoka katika stesheni ya Makutupola kupitia Isaka hadi Mwanza.

Kilimanjaro
Akizungumza katika Wilaya ya Same Magharibi Makalla anasema serikali imetoa Sh bilioni 59 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa kilometa 35 za barabara kutoka Same-Kisiwani-Mkomazi kwa kiwango cha lami.

Arusha
Nako mkoani Arusha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda alieleza Samia anakwenda kuufungua mkoa
wa Arusha kwa ujenzi wa barabara ambazo zitasaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi zikiwemo kilimo na utalii katika.

Makonda anasema katika barabara ya Tengeru-Usa River tayari mkandarasi ameshapatikani kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya njia nne kwa takribani kilometa 11.3. Anasema USA River wanaanza kujenga njia nne urefu wa kilometa 28 mpaka Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri kwa watu wanaotoka KIA Kwenda mjini.

Dar es Salaam
Makalla anasema maendeleo yaliyofanyika katika mkoa wa Dar es Salaam hayahitaji tochi ili mtu aweze kuyaona kwani Dar es salaam ya miaka kadhaa iliyopita si ya sasa na hata vumbi lililopo ni vumbi la maendeleo.

Makalla anaeleza hayo akigusia kuwa CCM inakwenda katika uchaguzi mkuu ikitembea kifua mbele kwa kuvunja rekodi ya maendeleo yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia akieleza miradi ya DMDP ambayo kwa sasa wilaya nne za mkoa wa Dar es Salaam wamenufaika nayo.

Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Abbas Tarimba anasema serikali imetoa Sh trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa miradi itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye Bonde la Mto Msimbazi katika Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam.

Makalla anasema moja ya vitu anavyowaahidi wananchi katika uchaguzi wa mwaka huu ni kuwa Ilani ya Uchaguzi
ya Mwaka 2025/2030 waliyoizundua imebeba matumaini kwani ina mambo muhimu yanayowagusa Watanzania.

Anasisitiza ilani imetokana na tathmini ya ilani iliyopita kwa kufanya utafiti na ushirikishwaji wa wananchi, asasi za kiraia na wadau mbalimbali ili kujua vipaumbele na mahitaji ya Watanzania na inakwenda kushughulika na ajira, kuimarisha uchumi, miundombinu na changamoto zote zinazowakabili Watanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button