‘Utumiaji akili bandia utatoa takwimu za haraka’

UTUMIAJI wa akili bandia na njia nyingine katika utafiti utawezesha kutoa takwimu za haraka ambazo zitawezesha serikali kufanya mipango ya maendeleo, ili kusaidia wananchi kutoka kwenye umaskini.

Mkurugenzi Mkuu wa Oxford Policy Management Tanzania, Dk Charles Sokile amesema leo wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa DEEP Challenge Fund Tanzania, ambao unalenga kuboresha mkakati wa kitaifa, sera, na programu zinazoathiri umaskini na mazingira magumu ya umaskini nchini Tanzania.

katika kufadhili watafiti na wachambuzi wa kitaifa ili kutoa maarifa na ushahidi unaoendana na mahitaji ya watunga sera.

Advertisement

Dk Sokile ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya DEEP, amesema mfuko huo umekuja na njia hiyo mbadala ya akili bandia ambayo inaweza kupima umaskini kwa haraka zaidi, kwa muda mfupi zaidi na kwa gharama ndogo zaidi.

“Kwa kutumia teknolojia kama akili bandia,  lengo ni kuwezesha watafiti na wataalam Watanzania waweze kushirikiana na wataalam wengine duniani kupima umaskini na kutoa takwimu ambayo itafanya sera za serikali ziweze kulenga zaidi umaskini na watu maskini na kuwasaidia watu wengi waweze kujikwamua katika hali zao za uchumi,” amesema.

Amesema wanatoa ufadhili huo kwa watafiti wa kitanzania kuwawezesha kujifunza njia hizo kwa kushirikiana na watafiti wengine duniani kuboresha, na wao kubuni njia nyingine kama wataweza kwa ajili ya kupima umaskini.

Amesema mfuko huo umezinduliwa kwa kusaidiana na Idara ya Uchumi ya Shule ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa upande wake Mtafiti mshauri kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Profesa Samwel Wangwe anasema kwa kipindi hiki miji inakuwa haraka zaidi kuliko ongezeko la watu.

“Miji ikikua, viwanda vinakua vinaleta ajira watu wanatoka vijijini wanakuja mijini kufanya kazi, wale wa vijijini nao kilimo chao kinaanza kuinuka kwa hiyo wanapata kipato kizuri kule au wanapata kipato kizuri kwenye viwanda.

“Sasa sisi viwanda haviongezi ajira inavyotakiwa, kule wakiondoka ni kama wanakimbia umaskini, lakini wanakuja kukutana na umaskini mwingine huku wa sekta ambayo sio rasmi kwa hiyo kote kunakuwa ni shida,” amesema.

Maelezo yake ni kwamba utafiti unapofanyika majibu wanayapeleka serikalini na kwenye sekta binafsi kwa kuwa wote wanahusika na maendeleo ya nchi.

Naye Winnie Muangi kutoka Shule Kuu ya Uchumi UDSM, amesema kwamba ufadhili huo watafiti wengi watapata uwezo wa kufanya utafiti mbalimbali katika maeneo tofauti ambayo yanasaidia.

“Kwa hiyo tunaona kabisa kuna pengo katika utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali iliyopo na pia kwenye tafiti ambazo zinasaidia kutoa taarifa jinsi gani hilo pengo linaweza kutatuliwa kwa ajili ya kusaidia maenendeleo,” amesema.