UVCCM watakiwa kuwa wabunifu miradi ya kimkakati

MKUU wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Sakina Mohamed amewataka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo kuwa wabunifu wa miradi yenye tija kwa maendeleo endelevu.

Sakina amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa ofisi za UVCCM Mbogwe na kueleza hatua hiyo itasaidia kuondokana na uchumi tegemezi ndani ya chama na kuwafanya vijana hao kuwa kioo cha jamii.

Amesema kupitia ubunifu wao, wanayo nafasi ya kuanzisha miradi itakayowapatia fursa kwenye miradi ya kimkakati na pengine kupata tenda tofauti ikiwemo katika ujenzi wa barabara na majengo ya umma.

Sakina amewasisitiza UVCCM kuwa mabalozi wa maadili ya kitanzania kwa kukemea na kukacha tabia hatarishi pamoja na kuhakikisha wanafanya suala la utunzaji wa mazingira kuwa ajenda ya kudumu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi UVCCM Mbogwe, Ferguson Masasi amesema ili kuondoa uchumi tegemezi wameanza kwa kujenga ofisi na kuanzisha miradi ya kufyatua tofari na studio ya picha.

Amesema miradi yote mitatu mpaka sasa imegharimu takribani Sh milioni 15 ambapo wamejipanga kuifanya UVCCM kuwa imara kiuchumi na kisiasa ili kuweza kujisismamia pasipo kutegemea mtu.

Ferguson amesema kwa kuanza amefadhili miradi hiyo kwa zaidi ya asilimia 90 kuhakikisha malengo ya UVCCM ya kuanzisha miradi inayounga mkono miradi ya kimkakati yanafikiwa ili vijana waweze kujiajiri.

“Hatujakomea hapa tutaendelea kushirikiana, tutaendelea kuwa na mawazo mengine, ambayo yatatufanya sisi tuweze kutoka kwenye hii hatua tuliyonayo tuende hatua zingine.” Amesema Ferguson.

Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Mbogwe, Mobahe George amesema ujenzi wa ofisi na uanzishaji wa miradi hiyo itawafanya kuwa siyo tu jumuiya ya chama bali pia kitovu cha maendeleo kwa vijana.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza la UVCCM mkoa wa Geita, Waziri Jumanne amekiri miradi hiyo itaondoa tabia ya ombaomba kwa UVCCM na kuwaweza kupanga na kutekeleza mipango thabiti.

Habari Zifananazo

Back to top button