Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mambo mazuri

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetoa wito kwa mashirika ya ndege ya ndani na nje ya Tanzania kutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwani ulinzi na usalama kwa ndege, abiria na mizigo umeendelea kuimarishwa kwa kuweka mifumo ya kisasa.

Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya jengo la tatu la abiria katika kiwanja hicho jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri David Kihenzile amesema uwepo wa usalama umeendelea kuwa na matokeo chanya kwani idadi ya mashirika yanayohudumiwa yamekuwa yakiongezeka ikiwemo Shirika la Ndege la Ufaransa na Shirika la Ndege la Saudia.

“Serikali inayongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuhakikisha miundombinu ya viwanja inaboresha na mashirika yanayongezeka kwenye viwanja vyetu,” amesema Kihenzile.

Amesema hivi karibuni wameongeza mashirika mawili ya nje na moja la ndani kutoa huduma kupitia kiwanja hicho na kwamba hiyo ni hatua kubwa.

Kihenzile ameipongeza TAA kwa kuendelea kusimamia viwanja vya ndege na kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa inapotokea changamoto za kiuendeshaji hali inayoongeza imani kwa abiria na mashirika ya ndege.

Amesema mipango ya serikali ni pamoja na kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la pili la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria zaidi ya milioni 3, badala ya milioni 1.5 waliokuwa wakihudumiwa kwa mwaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA Mussa Mbura, amesema mamlaka yake imejipanga kuhakikisha inaboresha zaidi viwanja vya ndege nchini ili kukuza utalii na kuongeza pato la nchi.

Naye Mkurugenzi wa JNIA, Mhandisi Rehema Myeya amesema kwa sasa jengo hilo la tatu la abiria linafanya kazi kwa saa 24 na abiria zaidi ya 2000 wanaweza kuhudumiwa kwa wakati mmoja.

Kihenzile yuko katika ziara ya siku tano jijini Dar es Salaam ya kukagua miundombinu ya uchukuzi.

Habari Zifananazo

Back to top button