Uwanja wa Uhuru umebeba makubwa ya Taifa

UWANJA wa Uhuru uliopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa viwanja vikongwe   ambavyo vina historia ya kipekee katika sekta ya michezo, ukiondoa ukweli kwamba ndipo ambapo Tanganyika ilisherekea kupata uhuru wake mwaka 1961. Nchi ambayo sasa ni Tanzania baada ya kuungana na visiwa vya Zanzibar  Aprili 1964.

Ni katika uwanja huo pia timu mbalimbali za mataifa yaliyoendelea kwenye soka kama England na Brazil zilifika na kucheza na klabu za hapa nchini katika miaka ya zamani na kwa hiyo ni uwanja ambao una historia ya kipekee.

Uwanja huo una rekodi kadhaa ambazo zimewahi kubeba furaha na huzuni za wanamichezo na timu zetu kwa nyakati tofauti katika miaka ya nyuma. Kwa muktadha huo uwanja wa Uhuru unabaki kuwa uwanja pekee ambao una kila sababu ya kuenziwa na kufanywa eneo la kumbukumbu ya michezo.

Ni katika uwanja huu pia matukio mbalimbali ya kitaifa kama sherehe za Maadhimisho ya Uhuru yamekuwa yakifanyika karibu kila Desemba 9 ya mwaka na hata sherehe za kumbuku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26 kila mwaka imekuwa ikifanyika kwenye uwanja huo.

Ibada ya mazishi ya Rais wa kwanza wa  Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ilifanyika uwanjani hapo Oktoba 21, 1999, Muda mfupi baada ya kifo chake. Aliyekuwa Rais wa awamu ya 5 hayati  Dk John Magufuli pia aliagwa katika uwanja huo Machi 21, 2021.

Historia inaonesha mwaka 1918, serikali ya kikoloni ya Ujerumani, ilijenga uwanja wa ndege katika eneo la Kurasini ulioitwa ‘Mkeja Aerodrome’ na ulijengwa katika eneo ambalo sasa kuna uwanja wa Uhuru, jirani na uwanja wa Benjamin Mkapa, Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) JKT Mgulani na Shule ya Sekondari Jitegemee, pamoja na Jeshi la Wokovu.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918), Wajerumani wakaondoka nchini na kuja Waingereza. Wao wakauhamisha Uwanja wa Ndege kutoka Kurasini hadi Ukonga.

Uwanja huo mbali na historia ya kutumika kwa matukio mbalimbali ya  kitaifa, una historia njema katika matukio ya kimichezo.

Mwaka 1979 Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa ikitumia uwanja huo kwenye michezo ya kimataifa ilifuzu kushiriki fainali za Afrika (Afcon) kwa mara ya kwanza katika fainali zilizofanyika Nigeria mwaka 1980. Pia, Simba na Yanga na timu nyingine zilikuwa zinautumia uwanja huo kwa mechi za nyumbani za kitaifa  na kimataifa.

Histori iliwekwa mwaka 1993 wakati uwanja huo ulipochezewa mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la CAF kati ya Simba na Stella Abidjan ya Ivory Coast, huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Simba ilifungwa mabao 2-0.

Uwepo wa uwanja huo umefanya  kutumika hadi sasa kwenye shughuli mbalimbali za kitaifa na hata zile binafsi, hata hivyo serikali imekuwa ikijitahidi kuukarabati uwanja huo, ili uendelee kudumu katika matumizi ya matukio ya kitaifa.

Kwa kuonesha umuhimu wa uwanja huo,  Aprili 25, 2024, mtandao wa HabariLeo uliripoti kuwa jumla ya Sh bilioni 19.7 zitatumika kukarabati Uwanja wa Uhuru Dar es salaam ‘Shamba la bibi’, kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu   Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati wa kusaini mkataba wa kuanza kwa ukarabati wa uwanja huo Dar es Salaam.

Ukarabati huo utafanywa na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ambapo watafanya kazi hiyo kwa kipindi cha miezi 12.

Uwanja wa Uhuru ni moja ya viwanja vilivyo katika mpango mkakati wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2027) ambapo Tanzania ni moja ya nchi wenyeji wa michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.

Miaka ya nyuma Uwanja wa Uhuru ulikuwa ukijulikana kama Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini baada ya kufunguliwa kwa Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam (Sasa Uwanja wa Mkapa), ndipo ukabadilishwa jina na kuitwa Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni kumbukumbu ya eneo ambao sherehe za uhuru zilifanyika Desemba 9, 1961 wakati wa kushusha bendera ya Mwingereza na kupandisha ya Tanganyika.

*Imeandaliwa na Brown Juma, Grace Mkojera na Rahim Fadhil.

Habari Zifananazo

Back to top button