Uwekezaji kilimo cha mbaazi uenziwe kuimarisha uchumi EAC

TANZANIA ni mzalishaji bora na mkubwa wa zao la mbaazi ikishika nafasi ya pili duniani baada ya India.

Hii ni fursa kubwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujipanga na kuitumia Tanzania kama kielelezo kwenye uwekezaji kwenye kilimo cha mbaazi.

Uzalishaji wa mbaazi nchini umeongezeka hadi kufikia tani 307,000 kwa msimu uliopita hali inayotoa motisha kwa mataifa ya Afrika Mashariki kuingia katika kilimo cha zao hili muhimu.

SOMA: Wakulima wapata Sh bilioni 32 mauzo mbaazi

Hivi karibuni, kwenye mkutano mkuu wa wadau wa korosho uliokuwa ukijadili mwenendo wa zao hili nchini kwa mwaka 2024/2025, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola alisema ongezeko hilo kwa msimu uliopita umeiweka Tanzania kwenye nafasi ya pili ya uzalishaji wa mbaazi duniani baada ya India.

Mkutano huo ulioangalia pia urasimishaji wa mifumo ya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko, umeleta matokeo chanya kwenye maendeleo ya uzalishaji na mnyororo wa biashara ya zao la mbaazi nchini.

Hatua hiyo imeleta tija kwenye kilimo cha mbaazi na kuhamasisha wakulima kuzalisha zaidi na kufanya uzalishaji wa mbaazi Tanzania kupanda hadi kufikia tani 400,000 msimu huu ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 90,000 katika miaka minne iliyopita.

Mbali na ongezeko hilo la uzalishaji wa mbaazi nchini, bei yake katika soko la dunia imepanda maradufu ikilinganishwa na bei ya nchini miaka mitatu iliyopita.

Mathalani, 2022/2023 wakulima waliuza kilo ya mbaazi kati ya Sh 200 na Sh 500 wakati soko la India lilinunua kwa zaidi ya Sh 2,200 na kwa sasa mkulima wa Tanzania anapata zaidi ya asilimia 66 ya bei ya soko la dunia.

Huu ni uthibitisho tosha kuwa ikiwa nchi za EAC zitawekeza kwenye uzalishaji wa kutosha wa zao hilo, matunda yake yatakuwa mengi kwa wakulima na uchumi wa kanda nzima kwa ujumla.

Tunaamini kuwa ardhi iliyozalisha mbaazi vizuri nchini, ni hiyo hiyo iliyopo katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na Somalia.

Kutokana na ukweli huo, ikiwa Tanzania imeweza kuzalisha tani 400,000 inawezekana mataifa ya EAC yakazalisha kwa kiwango hichohicho kwa sababu majira ya mvua katika nchi hizo yanafanana.

Ni ukweli kuwa mataifa manane ya EAC yanaweza kuzalisha tani milioni 3.2 za mbaazi kwa msimu hali itakayoiweka Jumuiya ya Afrika Mashariki katika nafasi bora ya kuilisha dunia mbaazi na kuingiza mabilioni ya Dola za Marekani.

Matamanio yetu ni kuona EAC ikinawiri kiuchumi na kuzalisha mazao mengi yatakayoleta ushindani katika soko la dunia kutokana na ubora na thamani yake.

Tunategemea kuwa Tanzania kama mwalimu na kiongozi mkuu wa EAC katika uzalishaji wa mbaazi, pia itaendelea kutoa soko katika mazao mengine kama korosho, kahawa, ufuta, zabibu na mazao mengine.

Jambo la muhimu ni kuona EAC kupitia sekretarieti yake inajihusisha moja kwa moja kuhamasisha uwekezaji kwenye kilimo ambacho ni rahisi kwa kila nchi kuweza kuwekeza na ambacho hakihitaji teknolojia kubwa kwenye uzalishaji wa mazao.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Hello there, just became alert to your blog through Google, and found that it is really informative. I’m gonna watch out for brussels. I will appreciate if you continue this in future. A lot of people will be benefited from your writing. Cheers!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button