DAR ES SALAAM; UJIO wa usafirishaji kwa pikipiki nchini umeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri, ukitoa fursa kwa wananchi chaguo la aina ya usafiri rahisi na wa haraka hususani katika miji yenye msongamano kama Dar es Salaam.
Bodaboda zimewezesha abiria kufika haraka katika maeneo yao ya kazi na shughuli nyingine kwa gharama nafuu, ikilinganishwa na usafiri wa magari mathalani daladala.
Hata hivyo, pamoja na faida mbalimbali za usafiri huu ikiwamo kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana, hali ya usafiri huu bado inakabiliwa na changamoto kwa sababu ya uendeshaji holela unaoshuhudiwa barabarani.
Wasafirishaji wengi hawafuati sheria za usalama barabarani, hivyo kuleta hatari kwa abiria na watumiaji wengine wa barabara. Takwimu zinaonyesha kuwa ajali za pikipiki zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Taarifa mbalimbali zinabainisha ambavyo ajali za bodaboda ni tishio kutokana na uvunjifu wa sheria na kanuni za usalama barabarani ambao hauishii kuhatarisha maisha ya wanaoendesha vyombo hivyo na abiria wao, bali pia waenda kwa miguu na madereva wengine.
Katika miji kama Dar es Salaam, ni kana kwamba vyombo hivi vimepewa ‘msamaha’ wa kutozingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwamo kuheshimu taa za barabarani na alama nyingine zilizowekwa.
Bodaboda zimejipa baraka ya kutumia hata vivuko vya waenda kwa miguu jambo ambalo linahatarisha maisha ya watumiaji.
Hivi karibuni, Mkuu wa Kituo cha kikanda cha umahiri katika usalama barabarani Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Godlisten Msumanje akiwa wilayani Kasulu, Kigoma, alikaririwa akitaja bodaboda kuwa ni tatizo katika kudhibiti ajali za barabarani hasa kwenye vivuko kutokana na kutozingatia sheria za usalama, jambo ambalo tunakubaliana naye.
Tunatambua juhudi za serikali katika kusimamia usalama barabarani. Hata hivyo, tunaunga mkono agizo la Kamishina wa Operesheni na Mafunzo katika Jeshi la Polisi, Awadh Juma Haji aliyotoa hivi karibuni mkoani Dodoma akiwataka wakuu wa usalama barabarani wa mikoa na wilaya kuongeza kasi katika usimamizi wa taratibu, kanuni na sheria kudhibiti madereva wanaokiuka sheria.
Akifungua kikaokazi cha wakuu wa usalama barabarani wa mikoa na wilaya kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Haji alisema usimamizi mdogo wa sheria za usalama barabarani husababisha kuwe na madereva wazembe wanaoendesha vyombo vya moto bila kuzingatia sheria.
Tunasisitiza mamlaka zinazohusika, ziunde mkakati maalumu wa usimamizi na kuboresha usafiri huu wa bodaboda usiendelee kuwa janga kutokana na kusababisha ajali nyingi.
Mpango huo maalumu ujielekeze katika kusajili kila msafirishaji wa bodaboda, ukaguzi wa mara kwa mara wa bodaboda, elimu endelevu kuhusu sheria za usalama barabarani na udhibiti wa wanaoendesha biashara hii holela bila kufuata utaratibu.
Ifike wakati kila mtumiaji wa barabara aheshimu sheria zilizowekwa. Suala la usalama wa barabarani na udhibiti wanaozivunja, lisiwe la kuwajibisha magari pekee hasa daladala, bali kila chombo cha moto. Hatimaye usafiri wa bodaboda usiwe wa holela unaohatarisha maisha ya watumiaji wote wa barabara.
@@@@@@@
Tahadhari zianze kwa mvua iliyotabiriwa
Na Amina Omari
MWANZONI mwa mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza maeneo ambayo yatapata mvua chini ya wastani hadi juu ya wastani sambamba na maeneo ambayo yataweza kuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa.
Vile vile ilitangaza maeneo ambayo yatakuwa na vipindi vya mvua kubwa na baadhi ya maeneo ambayo mvua hizo zinaweza kuleta athari ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Taarifa hiyo ilitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani ni pamoja na Kigoma, Kagera, Simiyu, Mara, Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba.
Hivyo, kutokana na taarifa hiyo, mamlaka za mikoa ambayo imetajwa zina wajibu wa kuchukua hatua za tahadhari mapema ikiwemo kuwahamisha watu kwenye makazi ambayo ni hatarishi kwani mvua hizo zinaweza kuleta kusababisha upotevu wa mali na maisha.
Ni muhimu mamlaka za mikoa zikajiandaa, hususani kwa kuimarisha timu za uokozi na idara ya afya na kinga kwani mara nyingi tumeweza kushuhudia mvua hizo licha ya athari za kimazingira, husababisha pia mlipuko wa magonjwa.
Hivyo ni vema kamati za afya kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa zikawa tayari kuchukua tahadhari mapema kwa ajili kukabiliana na milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu kwani bila hivyo madhara yake huwa ni makubwa zaidi.
Licha ya kamati za afya lakini wataalamu wa miundombinu ni vema kuanza kufanya ukaguzi wa uimara wa madaraja, barabara na kubaini njia za asili za maji kwa kuchukuwa tahadhari mapema ili kuepuka madhara yanayotokana na mvua hizo.
Nikirejelea mfano wa mvua za Elnino za mwaka jana, Mkoa wa Tanga ulishuhudia changamoto kadhaa ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na kukatika kwa madaraja hatua ambayo ilisababisha Waziri wa Ujenzi wa wakati huo, Innocent Bashungwa kufanya ziara ya kujionea athari za mvua hizo.
Matukio kadhaa yaliripotiwa, miongoni mwake ikiwa ni kukatika kwa barabara kutokana na mvua hizo katika eneo la Msente na Mswaki wilayani Kilindi na kusababisha wananchi kulala nje kwa siku kadhaa na wengine wakikosa huduma za kijamii.
Pia, baadhi ya maeneo ya Jiji la Tanga kama vile Donge, Duga pamoja na Magomeni, wananchi walilazimika kuhama maeneo yao baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji. Mali ikiwamo mifugo, zilisombwa na maji.
Hali iliyosababisha serikali kuchukua hatua za haraka kwa kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kuhudumia wananchi hao mpaka pale hali ya hewa ilipokuwa sawa.
Ni vyema wakati huu ambao tahadhari imeshatolewa, wananchi wa maeneo husika waanze kuchukua hatua mapema.
Licha ya mamlaka kuchukua hatua, pia wananchi hatuna budi kuanza kusafisha maeneo yetu kwa kuzibua mitaro na wale ambao wanaishi mabondeni waanze kondoka ili kuepuka madhara.
Vile vile kamati za afya ziimarishwe kuanzia ngazi ya vijiji kwa kuhakikisha zinasaidiana na serikali katika kutoa elimu ya tahadhari kwa wananchi. Lengo liwe ni kuhakikisha mvua hizo hazileti madhara makubwa.