“Uwezeshaji mabinti msingi mabadiliko ya jamii”

MJASIRIAMALI mashuhuri wa Tanzania, Bernice Fernandes ametoa wito wa kuchukua hatua za pamoja kukomesha ndoa za utotoni, akisisitiza kuwa zinachangia umasikini wa kizazi na kupunguza fursa za mabinti.

Akizungumza wakati wa hotuba yake kuu katika Kongamano la Kimataifa la Wanawake lililofanyika katika Tamasha la Ujasiriamali la Dunia (GEF), Fernandes amesema uwezeshaji wa mabinti ni msingi wa mabadiliko ya kijamii.

Advertisement

“Binti anapoozeshwa akiwa mdogo, anakwama katika maisha ya chaguzi finyu,” alisema Fernandes. “Anakua akiamini kuwa jukumu lake pekee ni kuzaa watoto na kusimamia familia, bila kutambua uwezo wake wa kufanya mambo makubwa zaidi.”

Kongamano hilo, lililokuwa na kaulimbiu “Kutokomeza Umasikini Bila Mipaka”, liliwaleta pamoja viongozi wa kimataifa, wajasiriamali, na wanaharakati kujadili mikakati ya kupambana na umasikini na ukosefu wa usawa.

Fernandes, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya GEF, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu na maendeleo ya ujuzi kwa mabinti ili kuwapa zana za kufanikiwa.

“Fikiria dunia ingekuwaje kama kila binti angepata fursa ya kujifunza, kubuni, na kuongoza,” aliongeza, akisema kuwa mabadiliko ya kijamii lazima yaanzie kwa kushughulikia ukosefu wa usawa unaowakumba wanawake na wasichana.

Katika hotuba yake, Fernandes pia alizungumzia ukosefu wa usawa kazini, akibainisha kuwa wanawake mara nyingi hupuuzwa katika nafasi za uongozi. Amewahamasisha wanawake kuwa na ujasiri wa kudai nafasi zao.

“Jitokezeni, chukueni nafasi, na dai kutambuliwa kwa mchango wenu,” alisema.

Mbali na hotuba yake, Fernandes aliongoza mjadala wa Women’s Power Panel, uliolenga ushauri nasaha, udhamini, na mitandao kama zana za mabadiliko ya jamii.

Juhudi zake katika tamasha hilo zilithaminiwa kwa tuzo ya utetezi na huduma yake katika Bodi ya GEF. Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Fernandes ametoa wito wa kuendelea kuweka juhudi za kufungua uwezo wa wanawake na wasichana.

“Wanawake ni viongozi wanaoweza kubadilisha dunia,” amesema, akiwaongoza washiriki kupigania mabadiliko na kujenga jamii yenye usawa zaidi.