Vijana 600 Sengerema, Ilemela kupata mafunzo ujasiriamali

ZAIDI ya vijana 600 kutoka Wilaya ya Sengerema na Ilemela mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika na mradi wa kuimarisha ujasiriamali na ajira kwa vijana (EYEE) unaosimamiwa na Shirika la kimataifa la kujitolea(VSO).

Hayo yamesemwa leo na mshauri wa shughuli za uwezeshaji wa vijana wa shirika la VSO, Eziboni Mnahi wakati wa mahojiano malumu na HabariLEO katika manonyesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo.

Akielezea zaidi kuhusu mradi wa EYEE, Mnahi amesema mradi huo una lengo kuu la kuwezesha vijana kuanzia umri wa miaka 18 mpaka 34 kushiriki katika shughuli za ujasiriamali kuanzia hatua za awali za uanzishaji wa biashara ili waweze kukua katika biashara kwa kuongeza kipato na wigo wa masoko.

Advertisement

‘’Mradi huu umefadhiliwa na taasisi ya Standard Chartered Foundation ambapo mradi ulianza mwaka 2021(awamu ya kwanza) na utamalizika mwaka Desemba 2023(awamu ya pili)’’ amesema Mnahi.

Amesema kupitia mradi huo vijana watanufaika na utoaji wa huduma za maendeleo ya biashara na mikakati jumuishi ya kifedha kupitia miradi ya mikopo.

Amesema mradi utajenga uwezo wa vijana pamoja na mitandao yao ya kibiashara kwa kuwashirikisha katika kufanya maamuzi kwenye fursa za ujasiriamali.

Amesema vijana wataunganishwa na huduma za kifedha zinazotolewa na Shirika la kuendeleza viwanda vidogo(SIDO).

Mnahi ameshukuru sana Idara ya maendeleo ya jamii na ofisi za kata katika maeneo mbali mbali kwa kufanya kazi kwa ushirikiano wa ukaribu sana na shirika lao.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *