Vijana kunufaika gharama nafuu pikipiki za umeme

VIJANA wanatarajia kunufaika na upatikanaji wa ajira na kupunguza gharama za uagizaji wa pikipiki nje ya nchi kutokana na Kampuni ya Spiro Africa kuwezesha upatikanaji wa pikipiki zinazotumia umeme.

Kampuni hiyo imezindua rasmi shughuli zake nchini ikiwa ni hatua ya kuongeza nguvu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini na ajenda ya nishati safi kwani pikipiki hizo zitakuwa zikitumia umeme na kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Spiro Kanda ya Kenya na Tanzania, Kshitij Sharma, alisema ujio wa kampuni hiyo nchini ni mchango wa kimkakati katika juhudi za taifa kufikia maendeleo endelevu.

“Ili kusaidia uchumi wa ndani, Spiro inapanga kuanzisha na kushirikiana na viwanda vya kuunganisha pikipiki nchini Tanzania. Hatua hii itachochea ajira, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, na kupunguza gharama na hivyo kufanya usafiri kupatikana kwa urahisi zaidi,” alisema Sharma.

Alisema kuwa tayari kampuni hiyo imeweka zaidi ya vituo 10 vya kubadilishia betri jijini Dar es Salaam, huku ikiwa na mipango ya kupanua zaidi mtandao huo.

“Kwa kuweka pikipiki za umeme na vituo vya kubadilisha betri katika maeneo muhimu ya Dar es Salaam kama vile Gongo la Mboto, Kariakoo, Kigamboni, Mbagala na Total Station Bonyokwa, Spiro inapunguza utegemezi wa mafuta na kuchangia hewa safi katika maeneo yenye msongamano mkubwa,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Spiro, Kaushik Burman alisema kuwa kampuni hiyo pia itaanzisha mikopo nafuu pamoja na mafunzo rasmi kwa vijana na wajasiriamali wadogo.

“Ahadi yetu ni kutoa usafiri wa gharama nafuu na rafiki kwa mazingira unaobadilisha mfumo wa usafiri mijini na kusaidia kukuza uchumi wa bara zima la Afrika,” alisema Burman.

Aidha, kampuni hiyo pia imepanga kushirikiana na taasisi muhimu za serikali kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), pamoja na kampuni za teknolojia ya kifedha na majukwaa ya usafiri kwa njia ya mtandao.

Ushirikiano huu unalenga kusaidia upanuzi wa miundombinu, njia za malipo kwa njia ya kidigitali pamoja na kuharakisha matumizi ya teknolojia safi ya usafiri.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button