Vijana wahadharishwa wapotoshaji Muungano

VIJANA wametakiwa wawe makini na waepuke taarifa potofu kuhusu historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964.
Waziri wa zamani katika Serikali ya Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo akiwasilisha mada kwenye Kongamano la Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania lililofanyika Dar es Salaam jana.
Dk Mwakyembe aliwasilisha mada kuhusu ‘Historia ya Muungano, tulipotoka, tulipo na tunapoelekea’.
Waziri huyo wa zamani alisema ni jukumu la vijana kuchukua tahadhari kuhakikisha maudhui yote wanayokutana nayo kuyapima usahihi wake kabla ya kuyabeba.
Alisema kutokana na tabia ya vijana kujishughulisha na intaneti muda mwingi, wako katika hatari ya kulishwa historia mbovu ya Muungano hali itakayowafanya kuwa na historia ya uongo kuhusu taifa lao pamoja na Muungano wa taifa lao.
“Madhara ya historia iliyopotoshwa ni makubwa kwa jamii kuliko hata madhara ya silaha za maangamizi au virusi vya Corona kwa sababu vyote hivyo ni vya muda mfupi tu lakini madhara ya upotoshaji wa historia ni ya vizazi na vizazi na yanaweza kudumu kwa karne kadhaa hadi wahusika watakapoamka na kurekebisha,” alisema Dk Mwakyembe.
Alifafanua kuwa ili kuokoa vizazi vijavyo na balaa la upotoshaji wa historia ya Muungano, ni wajibu wa viongozi na wanataaluma kusahihisha upotoshaji wote unaofanywa katika mitandao kupitia matamasha na makongamano.
“Ni wajibu wetu wanataaluma, viongozi na wazalendo wa taifa hili kubeba jukumu la kusahihisha maudhui ya historia potofu ya Muungano inayotolewa kwa malengo mabaya na watu wasioitakia mema nchi hii,” alisisitiza Dk Mwakyembe.
Aidha, Dk Mwakyembe alitoa siri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kudumu kwa muda mrefu ikilinganishwa na miungano mingine Afrika na duniani kwa ujumla, akisema cha kwanza ni nia na utashi wa kisiasa waliokuwa nao waasisi ambao ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amani Karume.
Akitolea mfano Muungano ulioshindikana kutokana na ukosefu wa utashi wa kisiasa, Dk Mwakyembe alisema lengo la Mwalimu Nyerere lilikuwa kuunganisha mataifa manne katika Shirikisho la Afrika Mashariki.
Alisema mataifa hayo yalikuwa ni Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar, lakini viongozi wa Kenya na Uganda hawakuwa na utashi wa kisiasa na kuamua kwenda na Mzee Karume ambaye alikuwa tayari.
Dk Mwakyembe aliishukuru serikali kupanga utaratibu wa kuanza kutoa elimu kwa vijana na rika mbalimbali kuhusu Muungano ili kukabiliana na upotoshaji mkubwa unaofanywa na watu wachache wenye nia mbaya na amani na utulivu wa nchi yao.



