Vijana wahimizwa kuunda vikundi vya ujasiriamali

MOROGORO: ZAIDI ya vijana 20,000 walioshiriki Tamasha la Sara Msafiri Festival 2026 wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, wamehimizwa kuunda vikundi vya ujasiriamali vilivyosajiliwa ili waweze kunufaika na fursa za mikopo ya Halmashauri na kujikwamua kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Richard Kasesela, wakati wa kufunga mashindano ya tamasha hilo yaliyofanyika katika Uwanja wa Turiani na kuhitimishwa Oktoba 17, 2026, baada ya kudumu kwa miezi miwili.

Kasesela amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Sara Msafiri, katika kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia michezo na vikundi vya ujasiriamali, akiwataka viongozi wa Halmashauri kushirikiana kuhakikisha fursa hizo zinakuwa endelevu.

Amesema mashindano hayo, yaliyoshirikisha timu kutoka vijiji 130 vya wilaya hiyo, yamekuwa jukwaa la kuwaunganisha vijana, kukuza vipaji na kuwajengea msingi wa kutumia uwezo wao katika kujiletea maendeleo.

Amehimiza madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kushirikiana na mbunge huyo katika maandalizi ya mashindano ya mwaka 2027 ili kuimarisha ushiriki wa vijana na kuongeza manufaa ya kijamii na kiuchumi.

“Kwa sababu Mheshimiwa Mbunge umefanya kazi kubwa kuwakusanya hawa vijana na kuwaunganisha, tunakupongeza. Huu ndio msisitizo wa Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, wa kuwapa tabasamu Watanzania,” amesema Kasesela.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mvomero, Sara Msafiri, amesema tamasha hilo limefanikiwa kuwakutanisha zaidi ya vijana 20,000 kutoka timu za vijiji vyote 130 vya wilaya hiyo, huku ofisi yake ikijiandaa kuboresha mashindano ya msimu ujao.

Amesema maboresho yanayopangwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya viwanja na kufunga taa za sola katika baadhi ya viwanja ili kurahisisha uchezaji na kupunguza changamoto ya mechi kukatishwa kutokana na giza.

Mmoja wa wachezaji wa timu ya Kata ya Mtibwa, Adam Carlos, amemshukuru mbunge huyo kwa kuwapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya ujasiriamali vilivyosajiliwa.

Katika fainali za mashindano hayo, timu ya Kata ya Mtibwa ilitwaa ubingwa wa Sara Msafiri Festival 2026 na kujinyakulia pikipiki mpya yenye thamani ya Sh milioni tatu, Sh milioni moja taslimu na ng’ombe mmoja aliyetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button