Vijana waomba ushiriki ngazi za maamuzi

DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema changamoto za ajira na kipato ni miongoni mwa sababu zinazochochea vijana kudai nafasi na mahitaji yao katika jamii.
Pia, kimeeleza kuwa vijana wanapaswa kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kutumia uwezo wao katika maendeleo badala ya kujieleza kupitia vitendo vinavyoharibu mali na miundombinu.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Utafiti), Profesa Nelson Boniface, amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Sauti ya Sayansi za Jamii ulioandaliwa na Ndaki ya Sayansi za Jamii ya chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku mbili ulikuwa na kaulimbiu isemayo ‘Kutafakari Upya Leo na Kesho: Kizazi cha Gen Z na Harakati za Kijamii Barani Afrika’, ukiwakutanisha watafiti na washiriki kutoka nchi mbalimbali kujadili changamoto na nafasi ya vijana katika jamii.
Alisema harakati za vijana zinaonekana duniani kote kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa ajira zinazoweza kuwachukua wahitimu wa vyuo vikuu na vijana wengine wanaotafuta kipato.
Alisema: “Idadi ya watu duniani imeongezeka na kuzidi uwezo wa uchumi kuzalisha ajira. Hivyo, sekta ya elimu, serikali na wafanyabiashara wanapaswa kushirikiana kutafuta shughuli za kuwawezesha vijana kupata kipato.”
Hata hivyo, alisema ingawa vijana wana haki ya kudai mahitaji yao, njia zinazohusisha uharibifu wa mali na miundombinu si sahihi, hivyo wazazi, walezi na wanataaluma wana wajibu wa kuwaelimisha njia bora za kufikisha madai yao kwa wenye mamlaka.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka masuala ya vijana, ujasiriamali, elimu na ujuzi kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Sayansi za Jamii ya UDSM, Profesa Christine Noe, alisema harakati za Gen Z ni suala la kimataifa linalohusisha masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo zinahitaji kueleweka kupitia tafiti zinazozingatia mazingira tofauti ya vijana.
Alisema mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na tabianchi yanaathiri maisha ya vijana, yakiwapatia fursa mpya lakini pia changamoto zinazohitaji jamii na watunga sera kuzitambua.
Alisema hakuna sababu moja inayoweza kueleza harakati zote za vijana kwa kuwa changamoto na fursa wanazokutana nazo hutofautiana kulingana na mazingira wanayoishi.
Aliongeza kuwa mjadala huo utasaidia kupata mawazo ya vijana wenyewe kutoka nchi mbalimbali ili kuelewa wanachopitia na namna ya kuwawezesha kushiriki katika maendeleo ya mataifa yao.
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM, Mwakigoye Diamond Stephen, alisema mkutano huo ni fursa muhimu kwa vijana kutoa maoni yao na kushiriki katika mijadala ya maamuzi yanayohusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alisema vijana wamekuwa wakionekana kutokuwa na uwezo wa kujieleza na kuwakilisha maslahi yao, jambo linalofanya baadhi yao kuamua kusimamia hoja zao wenyewe.
Alisema: “Kupitia mkutano huu, vijana watapata fursa ya kuonyesha kuwa wana uwezo wa kujisemea wenyewe na kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu maisha yao na maendeleo ya taifa.”
Aliongeza kuwa harakati za Gen Z zinajitokeza katika maeneo mbalimbali, yakiwemo siasa, uchumi na jamii, hivyo mkutano huo unaweza kuongeza nidhamu na kujiamini kwa vijana katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa UDSM, Zuleha Mohammed, alisema vijana wanapaswa kupewa elimu ya kutosha ili waweze kuleta mabadiliko chanya katika jamii bila kusababisha vurugu.
Alitoa wito kwa viongozi na jamii kwa ujumla kuwapa vijana kipaumbele katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ili wajione kuwa sehemu muhimu ya maendeleo.
Katika mhadhara mkuu wa mkutano huo, Profesa Mette Olwig wa Chuo Kikuu cha Roskilde nchini Denmark, alieleza namna mitandao ya kijamii inavyowasaidia vijana kujenga mitandao ya kimataifa, kupata fursa za kitaaluma na kuendeleza ushirikiano unaovuka mipaka.
Hata hivyo, alisema matumizi ya mitandao hiyo yanaweza kuleta shinikizo kwa vijana kujenga taswira fulani ili kuvutia wafuasi na kupata nafasi za kushiriki katika mafunzo na mikutano ya kimataifa.
Alisema baadhi ya vijana walieleza kuwa picha na machapisho ya matukio wanayohudhuria huwasaidia kutambulika na kupata fursa nyingine, lakini pia huongeza shinikizo la kuwa hai muda wote kwenye mitandao ya kijamii.
Profesa Olwig alisema changamoto nyingine ni matumizi ya mifumo ya kimataifa kama Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo wakati mwingine haizingatii tofauti za mazingira, uzoefu na uwezo wa vijana wa Kaskazini na Kusini mwa dunia.
Alisema ingawa mitandao ya kijamii na malengo ya pamoja vinaweza kuwaunganisha vijana duniani, havipaswi kufuta tofauti zao za ndani au kuendeleza mifumo ya ukosefu wa usawa iliyojengwa katika historia ya ukoloni.
Alisisitiza kuwa mshikamano wa vijana duniani unapaswa kujengwa kwa kuzingatia mazingira na uzoefu wao halisi ili kuhakikisha sauti zao zinawakilishwa kwa usawa.



