Vijana washauriwa kulinda amani

DODOMA: Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Ally Liwaka, ametoa wito kwa Watanzania hususan vijana kuendelea kulinda na kuitunza amani ya nchi ili kudumisha mshikamano wa kitaifa.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa amani, Liwaka amesema kuwa katika maisha kuna mambo mengi ambayo mtu anaweza kuyachagua au kuyaacha, lakini amani si jambo la kufanyia uchaguzi kwani ni msingi muhimu wa maendeleo na ustawi wa taifa.
“Tunapopewa mambo kumi ya kuchagua, kuna mambo ambayo tunaweza kuyaweka pembeni, lakini amani siyo jambo la kuchagua. Lazima ibaki kama ilivyo,” amesema Liwaka.
Aidha, amewaomba Watanzania kuendelea kujenga umoja, upendo na mshikamano ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye utulivu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kulinda amani na kuhamasisha mshikamano katika jamii.



