Vijana watakiwa kutumia fursa kujiletea maendeleo

Vijana watakiwa kutumia fursa kujiletea maendeleo

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amezitaka halmashauri zote nchini ziendelee kutekeleza agizo la serikali la kutenga maeneo rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki shughuli za uzalishaji mali, ili kuwaepusha na kero ya kufanya biashara kwenye maeneo hatarishi.

Ametoa agizo hilo leo Jumatano, Oktoba 12, 2022, alipozindua Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Gymkhana mkoani Kagera.

“Maeneo haya ni lazima yawe na sifa zinazoendana na shughuli zinazofanywa na vijana,” amesema.

Advertisement

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako ashirikiane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angela Kairuki, ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.

Mbali na agizo hilo, pia amewaasa vijana kutumia vizuri fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ambayo inayoikabili dunia kwa sasa.

“Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini na sisi wenyewe kwa idadi yetu ni soko tosha la bidhaa mbalimbali, tutumie vizuri fursa hii ya kuwa na rasilimali nyingi kujipatia kipato,” amesema.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa fursa nyingine kwa vijana ni uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani.

“Fursa hii ikitumiwa vizuri na kundi la vijana wataweza kunufaika na kusonga mbele kimaendeleo”.

Akizungumzia kuhusu suala la mitaji, Waziri Mkuu amesema kuna  mifuko mingi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, hivyo waitumie, ili kupata mikopo hususan mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri na kuwekeza katika miradi yenye tija.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, amesema maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanatoa fursa kwa vijana kukutana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji mali na uzalendo.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *