Vijiji 9 kunufaika na mradi wa maji Malangali
VIJIJI tisa vya Wilaya ya Mufindi vinatarajia kunufaika na mradi wa maji wa Malangali ambao ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa zaidi ya Sh bilioni 5.
Utakapokamilika, mradi huo utanufaisha zaidi ya wananchi 10,500 wa vijiji hivyo na kuwaondolea adha ya upatikaji wa huduma hiyo katika maeneo yao.
Hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo kati ya RUWASA na Mkandarasi Ndika Engineering LTD umeingiwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego aliyesisitiza uzalendo na uadilifu katika kuutekeleza.
Dendego alimtaka mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango bora vinavyoendena na thamani ya fedha zilizotolewa.
“Nawakumbusha kazi hii mliomba wenyewe na mlithibisha kuwa mnaweza, tunataka kuona uwezo na weledi wenu kupitia ubora wa kazi mtakayoifanya ili wana Iringa wapate maji safi na salama,” alisema.
Aliitaka pia kampuni hiyo kutoa ajira ambazo hazihitaji ujuzi kwa vijana walioko kwenye maeneo ya mradi ili nao wanufaike na fursa ya fedha hizo.
“Licha ya dhamira ya dhati ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani-miradi kama hio inatakiwa kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika kupitia ajira ndogondogo zisizohitaji ujuzi wanazoweza kuzifanya na hivyo kusaidia kuboresha maisha yao,” alisema.
Awali Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wa mkoa wa Iringa, Mhandisi Joyce Bahati aliishukuru serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan akisema wamapokea asilimia 100 ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo.
Alisema mradi huu ni miongoni mwa miradi 21 inayotegemewa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo kati yake baadhi yake imekamilika na kuanza kutoa huduma.
Mhandisi Bahati alizitaja kazi zitakazofanywa kupitia mradi huo wa Malangali kuwa ni pamoja na ukarabati katika vyanzo vya maji chakavu na ulazaji wa bomba za maji kwa umbali wa kilometa 131.
Zingine ni ujenzi wa matanki mapya mawili katika Kijiji cha Ihowanza na Tambala ng’ombe na ujenzi wa tanki katika mnara wa mita tisa katika kijiji cha Ihowanza la ujazo wa lita 100,000.