Vikosi vya ulinzi vyajizatiti kulinda amani nchini

VIKOSI vya ulinzi na usalama vimeahidi kuilinda amani iliyopo nchini ambayo ni chachu ya kielelezo cha umoja na mshikamano wa wananchi ambao kwa kiasi kikubwa umeifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani kwa muda wote.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Zanzibar, Brigedia Jenerali Said Khamis Said ambaye ni mkuu wa Brigedia Nyuki ya Zanzibar amesema hayo katika kilele cha matembezi ya amshaamsha ya vikosi mbalimbali vya majeshi katika uwanja wa michezo Mnazi Mmoja, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema vikosi vya ulinzi na usalama vimepewa majukumu makubwa ambayo ni kulinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mipaka yake kuona nchi inakuwa salama pamoja na watu wake na kuwapa nafasi ya kufanya shughuli za maendeleo na kukuza uchumi.

Alisema maadhimisho ya mwaka huu ni tofauti na miaka mingine ambayo yamejikita moja kwa moja katika kuhamasisha umoja na mshikamano kwa jamii.

“Tumekusanyika hapa tukiwa na vikosi vya majeshi kutoka SMZ na SMT kwa lengo la kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni siku ya furaha kwa sababu sauti ya wazawa ilipata mamlaka ya kujitawala na kuongoza taifa katika mambo mbalimbali, tukiongozwa na jemedari Abeid Amani Karume na sisi leo (jana) tunasimama na kusema mapinduzi yametukomboa,” alisema.

Aliongeza kuwa ni faraja ya kila mtu kufanya mambo yake bila bughudha yoyote kwa sababu ya ulinzi na usalama ambao ndio nyenzo kubwa ya amani na utulivu, hivyo wananchi wote wanapaswa kushirikiana katika kuhakikisha fursa iliyopo haipotei kama taifa kwa ajili ya maendeleo.

Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na jamii limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la uhalifu, hivyo kwa kiasi kikubwa wanajivunia mafanikio katika maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Zanzibar kwa kupiga hatua ya ulinzi.

Aidha, alisema katika mwaka mpya wa 2026 jeshi la Polisi limejipanga kuongeza ushirikiano wake na jamii katika kupambana na uhalifu huku wananchi wakisisitizwa kutii sheria bila ya kushurutiswa.

“Uhalifu haulipwi, wananchi wajiweke mbali nao kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama tunaendelea kuweka mikakati mizuri kuhakikisha tunaendelea kuwa na amani katika taifa letu muda wote, hivyo wakati tuko katika kilele cha maadhimisho haya tuendelee kuhakikisha amani itaendelea kutawala,” alisema.

Mapema akizungumza Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo, Azzana Hassan Msingiri alisema wapiganaji wa SMZ na SMT wataendelea kuwa watiifu kwa kuhakikisha wanaendelea kulinda nchi kwa ushirikiano mkubwa kulingana na viapo vyao.

Kwa mfano kikosi cha KMKM kimejipanga kuongeza ulinzi wa baharini kwa kupambana na maharamia ambao hutumia usafiri wa baharini kwa ajili ya kuingiza na kusafirisha bidhaa za magendo kinyume na sheria ambazo huikosesha serikali mapato.

“Tunasherehekea kwa mtindo wa kipekee Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa sababu haya ni mapinduzi halali na kulingana na viapo vyetu vya kijeshi tutahakikisha tunalinda nchi na mipaka yake kwa ulinzi madhubuti na usio na mashaka, lengo ni kumfanya kila mtu aishi kwa amani na utulivu,” alisema.

Maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar yalifikia kilele chake Januari 12, mwaka huu ambapo wanajeshi na wapiganaji wa vikosi vya ulinzi na usalama walifanya matembezi maalumu kutoka Kambi ya Mtoni mpaka Uwanja wa michezo Mnazi Mmoja ambapo vikosi saba viliungana katika matembezi hayo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button