Viongozi Urambo wajifunza biashara ya hewa ukaa

Timu ya viongozi 38 wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora ikijumuisha madiwani pamoja na wataalamu wamefanya ziara mkoani Katavi Wilaya ya Tanganyika kwa lengo la kujifunza namna ambavyo Halmashauri imetekeleza na kunufaika na biashara ya hewa ukaa.

Akizungumza mara baada ya kupata elimu na baadaye kutembelea Zahanati inayojengwa katika Kijiji cha Kagunga,moja kati ya miradi inayotekelezwa kwa fedha zitokanazo na uvunaji wa hewa ukaa Wilayani Tanganyika, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Adam Malunkwi amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza ili kutanua wigo wa ukusanyaji wa mapato.

“Tumefika hapa kwenu kwa maana ya kuja kujifunza ,ziara yetu imekuwa yenye mafanikio ya kutosha kwa sababu tumejionea kwa macho, tumeshapewa darasa zuri sana kule wilayani tumefundishwa, tumeelewa na hapa tumejionea kwa macho namna ambavyo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imenufaika kupitia biashara ya Hewa Ukaa hongereni sana. Kilichobaki hapa ni kutekeleza kwa vitendo kile ambacho tumejifunza ”Amesema Mwenyekiti Malunkwi.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kutoka mkoani Tabora wamefurahishwa kwa namna ambavyo wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wamenufaika kupitia mradi wa Uvunaji wa Hewa Ukaa katika misitu inayomilikiwa na vijiji pamoja na Halmashauri wilayani humo.

Athumani Mwinyiko mmoja wa Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo amesema ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Tanganyika kuendelea kutunza misitu ili kuendelea kunufaika na biashara ya Hewa Ukaa.

“Bahati nzuri wameanza hatua ya chini na sasa wamepiga hatua kubwa, kama Halmashauri imefanikiwa kupata zaidi ya Bilioni 4 kwa mwaka kupitia mradi mmoja wa hewa ukaa, ukijumlisha na miradi mingine maana yake mapato yatakua juu zaidi ukilinganisha na Halmashauri zingine ambazo hukusanya mapato chini ya Bilioni 1” amesema Diwani Mwinyiko.

Naye Diwani wa Viti Maalumu kutoka Tabora aliyejitambulisha kwa jina moja Kamende, amesema wataitumia vyema elimu waliyoipata kuanzisha biashara ya Hewa ukaa kwa kuwa Wilaya ya urambo imebarikiwa kuwa na misitu ya kutosha.

“Wilaya ya Urambo tuna misitu mizuri lakini hatuifanyii kazi maana mnaweza mkawa na kitu lakini hamjui kukitumia, tumeona namna wanavyonufaika na Hewa ukaa na sisi niahidi tutaifanyia kazi elimu hii na tutawazidi hadi walimu” Amesema Diwani huyo kutoka Uyombo huko Urambo.

Awali akiwasilisha mada ya mradi wa Hewa Ukaa, Ofisa Maliasili na usafi wa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bruno Nicoulaus amewaambia Madiwani na wataalamu kutoka Wilaya ya Urambo kuwa, ili waweze kunufaika na biashara ya Hewa Ukaa ni muhimu kujipanga vyema kutunza misitu pamoja na kuimarisha ulinzi dhidi ya wavamizi mbalimbali ikiwemo majangili.

Ameongeza kuwa ni muhimu kuzingatia muongozo wa Kitaifa wa uanzishaji wa biashara hiyo ya hewa ukaa na pia kuwa makini katika uandaaji wa mikataba ya biashara hiyo ili iweze kuleta manufaa zaidi kwao.

Biashara ya hewa ukaa wilayani Tanganyika ilianza mwaka 2018 ikiendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ,Taasisi ya CARBON Tanzania kwa kushirikiana na mradi wa Tuungane kwa Afya na mazingira bora ukitekelezwa katika jumla ya vijiji nane ambavyo ni Lugonesi,Mwese,Lwega,Bujombe,Kapanga,Katuma,Mpembe, na Kijiji cha Kagunga.

Aidha mradi huo unahusisha misitu ya vijiji yenye ukubwa wa hekta 216,944 za ardhi katika vijiji vyote ambapo wakazi zaidi ya 34,242 wamefaidika na mradi katika sekta za Afya, Elimu na kuwezesha vikundi vya ujasiriamali.

Habari Zifananazo

Back to top button