Viongozi wa dini washauriwa kuepuka siasa nyumba za ibada

DAR ES SALAAM: VIONGOZI dini nchini hususan wachungaji, wamehimizwa kuheshimu mamlaka zilizopo kwa kutambua kuwa mamlaka hizo zimewekwa na Mungu, hivyo waepuke kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, muandaaji wa Tamasha la Pasaka na Krismasi, Alex Msama, alisema ni muhimu kwa watumishi wa Mungu kutofautisha kati ya kazi ya kiroho na masuala ya kisiasa.
“Huwezi kutumikia mabwana wawili. Kama umeamua kuingia kwenye siasa, basi acha uchungaji. Vivyo hivyo, ukiwa mchungaji, acha siasa,” amesema Msama.
Amesisitiza kuwa majukwaa ya kiroho yanapaswa kutumika kwa ajili ya kuhubiri Injili, kuwahimiza watu kuacha maovu, na kuwaongoza kumrudia Mungu ili taifa liendelee kuwa na upendo na amani.
Akirejea maandiko matakatifu katika Warumi 13, Msama alisema wale wanaohasi mamlaka waliowekwa wanamhasi Mungu mwenyewe. “Maandiko yanasema wazi kuwa washindanao na mamlaka wanashindana na Mungu, na siyo na mamlaka hizo pekee.”
Amesisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mteule wa Mungu, hivyo kupinga uongozi wake ni sawa na kumpinga Mungu.
“Katika Mathayo 2:16 tunaona mfano wa Mfalme Herode, na Warumi 13:5-7 inatufundisha juu ya wajibu wetu wa kutii mamlaka, kulipa kodi, na kuwa wanyenyekevu kwa kuwa viongozi ni watumishi wa Mungu walioteuliwa kutuongoza,” ameongeza Msama.
Mwisho, alitoa wito kwa viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika kujenga taifa lenye mshikamano, maadili mema, na maendeleo ya kweli.